HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 03, 2021

TMA: Ukame kuikumba mikoa 16 Tanzania


Ramani ya Tanzania inayoonesha maeneo yatakayopata mvua za chini ya wastani hadi wastani

 

 

Dk. Hamza Kabelwa (aliyesimama mbele) akizungumza na wanahabari kuhusu utabiri wa msimu wa Vuli kwa mwaka 2021.


Na Irene Mark

MIKOA 16 kati ya 31 hapa nchini inatarajiwa kupata ukame wakati wa msimu wa vuli unaoanza Oktoba hadi Disemba mwaka 2021.

Mikoa hiyo ni ile inayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka ambayo ni Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara na kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma kwenye Wilaya za Kibondo na Kakonko.

Mingine ni maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki (Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro), Pwani ya kaskazini (kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, mikoa ya Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga, na visiwa vya Unguja na Pemba.

Hayo yamesemwa Dar es Salaam leo Septemba 2.2021 na Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Hamza Kabelwa kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo Dk. Agnes Kijazi.

Ukame unaotarajiwa mwaka huu unalinganishwa na ule wa mwaka 2005 hivyo kuzitaka mamlaka mbalimbali za seikali na wananchi kuchukua hatua za tahadhari dhidi ya ukame huo.

Akizungumza na wanahabari, Dk. Kabelwa ametaja baadhi ya athari zitakazojitokeza kuwa ni upungufu wa unyevunyevu katika udongo unatarajiwa kwenye maeneo mengi ya nchi.

“Kujitokeza kwa magonjwa ya mlipuko kutokana na upungufu wa maji safi na salama pia upungufu mkubwa wa malisho ya wanyama na maji unaweza kujitokeza hivyo kusababisha migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.

“...Uwezekano wa kutokea matukio ya moto katika mapori na misitu upo hivyo mamlaka husika zinashauriwa kupanga mikakati mahsusi ya kukabiliana na hali hiyo,” amesema Dk. Kabelwa.

Alitumia fursa hiyo kuzitahadharisha mamlaka za Nishati, Maji na Madini kuhusu upungufu wa kina cha maji katika mito, mabwawa na hifadhi ya maji ardhini unatarajiwa kujitokeza hususan katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za chini ya wastani.

Amesema hali hiyo inaweza kupunguza upatikanaji wa maji kwa matumizi mbalimbali, uzalishaji wa madini (hususan dhahabu kwa wachimbaji wadogo) na nishati ya umeme utokanao na maji unaweza kuathirika.

Dk. Kabelwa amewataka wadau kuzingatia matumizi endelevu ya maji katika shughuli za kuchakata madini, uzalishaji wa umeme, matumizi viwandani na majumbani pia.

No comments:

Post a Comment

Pages