Baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere.
Baadhi ya wajumbe wa bodi.
Na Mwandishi Wetu
BODI
ya Wakurugenzi ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), inayomaliza muda
wake imemteua Joseph Butiku kuwa mwenyekiti mpya wa bodi hiyo.
Hayo
yamesemwa na Kaimu Mwenyekiti wa bodi aliyemaliza muda wake, Jaji
mstaafu Joseph Warioba jana wakati akiitambulisha bodi mpya ambayo
itakuwa na wajumbe 10.
Warioba
alisema bodi iliyomaliza muda wake ambayo ilikuwa inaongozwa na Balozi
Dk.Salim Ahmed Salim imefanikiwa kwa kiasi chake hivyo wanaamini kuwa
bodi mpya itaendeleza mazuri waliyofanya.
Alisema
Hayati Mwalimu Julius Nyerere alianzisha taasisi hiyo mwaka 1996 ikiwa
haina fedha ila walijitahidi kusuluhisha migogoro ya ndani na nje ambapo
moja ya mgogoro waliofanikiwa ni wa Burundi.
Alisema wamekuwa wakipitia changamoto mbalimbali ila wanashukuru wameweza kuzivuka.
"Tangu
mwaka 1996 tumekuwa tukishiriki kwenye mazungumzo ya maridhiano ambapo
mengi ya mazungumzo yameweza kufanikiwa ni imani yetu kuwa bodi mpya
ambayo ina wajumbe wa zamani wawili itaendeleza utaratibu huo kwa
maslahi ya Tanzania na Afrika kwa ujumla," alisema.
Warioba
alitoa rai kwa Watanzania kuiunga mkono bodi hiyo mpya ili iweze
kutimiza malengo hayo ambayo mwasisi wake Hayati Nyerere aliyasisi.
Kaimu
Mwenyekiti huyo, alitaja wajumbe wapya wa bodi ni Profesa Tarsis
Kabwegijere, Balozi Amina Salum Ally, Neema Nyerere, Geoffrey Israel,
Catherine Mgenda, John Kyaruzi, Balozi Celestine Liundi, Profesa Penina
Mlama na Profesa Martha Koro.
Akizungumza
baada ya kutangazwa kuwa mwenyekiti mpya wa bodi hiyo, Butiku alisema
mipango yake ni kuhakikisha dhana ya amani, umoja na maendeleo kwa kasi
ambayo italeta mabadiliko chanya kwa wananchi na nchi
Butiku
ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa MNF alisema katika uongozi wake
atahakikisha kasi ya kudumisha umoja, mshikamano na maendeleo
inafanikiwa.
"Mimi nipo
kwenye hii taasisi tangu 1996 malengo na matarajio yake nayajua na
nimekuwa nikiyatekeleza naamini nafasi hii itanipa nguvu zaidi kusukuma
mbele zaidi," alisema.
Butiku
alisema taasisi hiyo itahakikisha malalamiko yote ya kisiasa, kijamii,
uchumi na maendeleo yanapata muafaka kwa njia shirikishi kwani ndio
lengo la Hayati Nyerere.
No comments:
Post a Comment