Mkuu wa wilaya ya Muleba Mkoani Kagera Toba Nguvila.
Na Lydia Lugakila, Muleba
Kutokana na maelekezo yaliyotolewa ngazi ya Mkoa wa Kagera na Wilaya Muleba, kwa kuzingatia Sheria za Serikali za Mitaa kifungu cha 14 kipengele cha 2 na kifungu cha 15 kipengele cha 1 na na cha 2 watu wote waliovamia kwenye vitalu vya Ranchi ya Kagoma kinyume cha sheria, taratibu na kanuni wameondolewa na zoezi hili limekamilika kwa kuhusisha vikosi vya usalama.
Akizungumza wakati alipotembelea eneo hilo kuona namna zoezi hilo linavyofanyika, Mkuu wa wilaya ya Muleba Mhe. Toba Nguvila alivisisitiza vikosi vya usalama vilivyokuwa katika operesheni ya kuwaondoa wakazi wasio rasmi kwenye maeneo ya vitalu vya Mifugo kufuata utaratibu ili amani iweze kuendelea kuwepo katika kata ya Rutolo iliyopo katika eneo la ranchi ya Kagoma.
"Sihitaji machafuko kwenye wilaya ya Muleba na sihitaji mauaji kwenye wilaya ya Muleba. Hatuwezi kila siku tukawa tunashinda Rutoro, ni lazima ifike hatua tuweke utaratibu mzuri baina ya wewekezaji na wananchi wazawa ili amani iwepo", ameeleza Mhe Nguvila.
Aidha, ameongeza kwa kusema kuwa vijiji vya Rutoro, Kyobuheke, Byengeregere na kijiji cha Misambya ni vijiji ambavyo vinafahamika na vipo kwa mujibu wa sheria ambapo amesema kuwa katika vijiji hivyo kama kuna maeneo ambayo yana watu na kaya zipo nyingi watabaki ila kwa wale ambao wako katika maeneo ya kujitenga kwa maana nyumba moja moja watahamishwa warudishwe kwenye maeneo yenye watu.
Pia amewahimiza watu wa NARCO kuhakikisha wanajiridhisha na usalama wa eneo kwa kuhakikisha wanachunguza na kutambua watu wanaowapangisha ni watu wa aina gani ili kuweza kuepukana na mapungufu yanayoonekana sasa ikiwemo migogoro kati ya wafugaji na wakulima.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Muleba Ndg. Athuman Kahara amewaomba Kampuni ya NARCO pamoja na wawekezaji kuwa wazalendo kuhakikisha na wao wanashiriki kwa namna mbalimbali katika kuchangia maendeleo ya wananchi na wilaya kwa ujumla.
Baada ya zoezi la kuwaondoa watu waliovamia katika vitalu kukamilika tarehe 08.01.2022. Katibu Tawala Mkoa wa Kagera Profesa Faustine Kamuzora kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera alifanya kikao na kukutana na wajumbe wa Kamati ya Usalama ya Mkoa, wajumbe wa Kamati ya usalama ya Wilaya ya Muleba na Karagwe, Wenyeviti wa Chama cha Mapinduzi wa wilaya ya Karagwe na Muleba, Mbunge wa jimbo la Muleba Kaskazini Mhe. Charles Mwijage, wataalam na wawekezaji wenye vitalu Kagoma ranchi.
Akisoma taarifa ya zoezi hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Juma Haji Awadhi ameeleza kuwa zoezi limefanyika kuanzia tarehe 04.01.2022 hadi 08.01.2022 kwa vitalu 10 vilivyokuwa vimevamiwa, idadi kubwa ya wavamizi walikutwa tayari wameshaondoka na kuacha makazi yao. Ushirikiano mkubwa umetolewa baina ya wawekezaji na wakazi wazawa na hakuna madhara yoyote yaliyotokea.
Akizungumza katika kikao hicho Profesa Kamuzora amevishukuru vikosi vya usalama vilivyoshiriki katika zoezi la kuwaondoa watu waliovamia maeneo ya vitalu na kueleza kuwa kazi imefanyika kwa amani hakuna waliojeruhiwa wala hakuna damu iliyomwagika.
"Nawapongeza sana vikosi vya usalama vilivyoshiriki katika zoezi hili. Operesheni hii imekuwa tofauti na operesheni zingine. Kama tulivyosikia katika ripoti yetu, wavamizi wengi waliokuwa wamevamia maeneo ya wawekezaji wamekutwa tayari wameshaondoka kwa hiari yao kwenye maeneo waliyovamia. Hakuna damu iliyomwagika wala hakuna majeruhi," ameeleza Profesa Kamuzora.
Ameendelea kueleza kuwa baada ya zoezi la kuwaondoa wavamizi lengo la kikao ni kuanza kuwapanga wananchi waliondolewa katika maeneo yaliyobainishwa kitalu na 2 na kitalu namba 10 zoezi ambalo Mkuu wa Wilaya ya Muleba ametakiwa kulisimamia lifanyike ndani ya siku chache kabla ya wavamizi hawajarudi tena.
Naye Mhe. Nguvila amewasihi wawekezaji waache kupangisha watu wengine na wafanye shughuli za uwekezaji wenyewe kwani wakati mwingine wapangaji wa vitalu wanaowapangisha ndio chanzo cha migogoro baina ya wakulima na wafugaji. Sambamba na hilo ameomba kampuni ya NARCO iangalie namna ambavyo itaweza kupunguza ukubwa wa maeneo kwani vitalu ni vikubwa sana kiasi ambacho kutoka kitalu kimoja hadi kitalu kingine unatumia muda mwingi.
Kwa upande wake Mhe. Charles Mwijage, Mbunge wa Jimbo la Muleba Kaskazini, ameeleza kuwa pamoja na changamoto zote makubaliano yaliyofikiwa wakati wa kikao cha Waziri wa Mifugo na Uvuvi (Komuniki) yafuatwe lengo ikiwa ni kuzuia mauaji yasitokee na amani itawale.




No comments:
Post a Comment