Na Asha Mwakyonde, Dodoma
JUMLA ya shilingi bilioni 71, zitatumika kukamilisha mradi mkubwa wa ujenzi wa nyumba za makazi 1000 katika jiji la Dodoma awamu ya kawanza unaotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC),
Awamu ya kwanza ya mradi huo unaotekelezwa na shirika hilo ulianza Januari 6, 2021 katika eneo la Iyumbu yenye nyumba 404 ambao itagharimu shilingi bilioni 21 .4 na kukamilika Machi mwaka huu na Chamwino ambao ulianza Februari 1, 2021 na awamu ya pili itahusisha ujenzi wa nyumba 325 na majengo sita (6), ya kutoa Huduma na awamu ya tatu itakamilisha ujenzi wa nyumba 275.
Hayo yamesemwa leo Machi 8, 2022 jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk. Allan Kijazi wakati wa ziara ya kutembelea mradi huo wa nyumba 1000 zinazojengwa na NHC, amesema kuwa ikuwezesha ujenzi serikali iliipatia shirika hilo mkopo nafuu wa shilingi bilioni 20 zitakazotumika kama mtaji (Revolving Fund).
Dk.Kijazi ameeleza kuwa mkopo huo ni wa miaka 15 ambao utalipwa kwa muda wa miaka 12 baada ya miaka 3 ya kipindi cha ujenzi wa mradi huo wa nyumba 1000.
"Azma ya serikali ni kuliwezesha shirika la NHC kujenga nyumba hapa Dodoma ili kusaidia upatikanaji wa makazi na hasa baada ya uamuzi wa serikali kuhamishia shughuli zake jijini Dodoma," amesema Dk. Kijazi.
Amefafanua kuwa fedha hizo za mkopo huo wenye riba nafuu ya silimia 6.75 zimetolewa na baenki ya Azania na kwamba imekubali kuwakopesha wanunuzi wa nyumba za Iyumbu kwa riba nafuu ya asilimia 9.
Katibu huyo amesema shirika litaendelea kujenga za awamu ya pili na ya tatu kwa kutumia fedha zinazopatikana baada ya kuuza ambazo zimeshakamilika.
Amebainisha kuwa nyumba 101 zinazojengwa eneo la Chamwino ambazo zitapangishwa na nyumba 303 za Iyumbu zitauzwa kwa wananchi wanaohitaji.
" Nyumba zinazojengwa Iyumbu zipo za aina tatu ambazo nyumba za vyumba viwili zenye ukubwa wa mita za mraba 75 zipo 50, nyumba za vyumba vitatu zenye ukubwa w mita za miraba 100 zipo 100 na vyumba vitatu zenye ukubwa wa mita za miraba 120 zipo 150.
Amesema kuwa mradi wa ujenzi wa nyumba hizo mkoani Dodoma umewezesha upatikanaji wa ajira katika awamu ya kwanza ya mradi huo kwa eneo la Chamwino na Iyumbu na kwamba shirika hilo limewezesha ajira hizo za moja kwa moja 600 kwa siku ambazo zina shughuli nyingi za ujenzi na hupungua kadri shughuli zinavyopungua.
Awali Meneja Mradi wa NHC Frank Mambo anayesimamia nyumba 1,000 katika eneo la Iyumbu na chamwino amesema mradi huo utagharimu sh.bilioni 71 hadi kukamilika kwake na kufafanua kuwa katika awamu ya kwanza yenye nyumba 404 itagharimu sh.bilion 21.4 huku ukiwa unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Mei mwaka huu.
No comments:
Post a Comment