HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 14, 2022

KAMATI YA AMANI KUFANYA KONGAMANO LA MAOMBI KESHO


Na Julieth Mkireri, KIBAHA



KAMATI ya Amani ya Mkoa wa Pwani inatarajia kufanya kongamano la siku moja kwa ajili  ya kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan  pamoja na kuiombea nchi iendelee kudumu kwenye amani.


Wakizungumza na waandishi wa Habari viongozi wa kamati hiyo walisema kongamano hilo ambalo linatarajia kufanyika Machi 15 mjini Kibaha litashirikisha watu zaidi ya 200.


Mwenyekiti mweza wa kamati ya Amani Shekhe Hamis Mtupa alisema katika kongamano hilo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge ambapo viongozi wa dini watamuomba Mungu kwa ajili ya Rais Samia na pia  kuiepusha nchi na majanga.


"Sisi viongozi wa dini wa kamati ya amani tuliketi pamoja tukakubaliana mwezi wa tatu ni mwezi wa maombi, kumuombea Rais wetu, kuiombea nchi na kuombea majanga yanayoikabili nchi yetu" alisema.


Shekhe Mtupa alisema eneo la kwanza ambalo watafanya ni kuiombea Tanzania kuwa nchi ya amani kila mmoja kunyoosha mikono kumuomba Mungu kwa imani yake.


Alisema jambo lingine ni kuhusiana na chanjo ya UVIKO-19  wananchi waendelee kujitokeza kupata chanjo ikiwa ni mapambano ya ugonjwa huo lakini pia katika zoezi la sensa ambalo linatarajia kufanyika mwaka huu.


Naye Mchungaji Emmanuel Mhina akizungumza kwa niaba ya Mwenywkiti mweza wa kamati hiyo Beno Kikudo  alisema wameandaa kongamano hilo baada ya kushuhudia juhudi anazozifanya Rais Samia kuijenga nchi bila kukata tamaa.


" Kama viongozi wa dini tumeshuhudia anayoyafanya Rais wetu  kwa nchi bila kuchoka wala kukata tamaa imetusukuma kuandaa kongamano hili kumuombea Mungu amtunze katika kuliongoza Taifa letu" alisisitiza.


Mchungaji Mhina alisema watatumia nafasi hiyo kuwahamasisha wananchi ambao hawajapata chanjo kufanya hivyo kwa afya zao, lakini pia watawakumbusha kuhusiana na sensa wawe tayari kujitokeza kuhesabiwa.


Viongozi hao wamesema wanafanya kongamano hilo wakihusisha mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa madarakani.

No comments:

Post a Comment

Pages