HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 14, 2022

KUNENGE AZINDUA OPARESHENI WAHAMIAJI HARAMU PWANI


Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, akizungumza wakati wa uzinduzi wa oparesheni maalumu ya kudhibiti wahamiaji haramu.


 

 

Na Julieth Mkreri, KIBAHA

MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amezindua oparesheni maalumu ya kudhibiti wahamiaji haramu ambapo pia ameonya Maofisa wa Uhamiaji kutojihusisha  na rushwa katika oparesheni  hiyo.

Uzinduzi huo umefanyika jana mjini Kibaha ambapo oparesheni itatekelezwa katika maeneo mbalimbali ambayo yamekuwa yakitumika kama njia za Wahamiaji kuingilia kwenye mkoa huo.

Kunenge  alisema hatamvumilia  Afisa atakayebainika kujihusisha na vitendo vya rushwa wakati oparesheni hiyo ikitekelezeka na badala yake hatua za kisheria dhidi yake.

Mkuu huyo wa mkoa alisema Wahamiaji ambao wamekua wakiingia kinyume na utaratibu baadhi yao wanadaiwa wakijihusisha na vitendo vya uhalifu hali ambayo inahatarisha usalama wa wa wananchi kwenye maeneo husika.

Kunenge alisema kufanyika kwa oparesheni hiyo itasaidia kupunguza vitendo hivyo na kuuweka  mkoa uendelee kuwa salama na amani  alitumia nafasi hiyo kuwaomba wamiliki wa viwanda katika mkoa huo kutoa ushirikiano kwa Maofisa wa Uhamiaji watakapotembelea maeneo yao.

"Niwaombe wakuu wamikoa wenzangu kutoa ushirikiano katika oparesheni hii maana wapo wanaopita mikoa ya jirani wanakamatiwa Pwani ni wazi wapo watu wanawasaidia njia za kupita katika hili tukishirikiana kwa pamoja tutakomesha hii hali" alisema Kunenge.

Ofisa Uhamiaji mkoa wa Pwani Omari Hassan alisema oparesheni hiyo itafanyika kwa siku kumi ambapo imeanza jana Machi 14 hadi 23 huku shabaha kubwa ikiwa ni kudhibiti wahamiaji haramu.

Alisema Pwani ina fursa nyingi za kiuchumi ikiwemo viwanda vingi vilivyopo na vinavyoendelea kujengwa  na miongoni mwa wageni  wanaoingia na vibali halali  kuja kufanya kazi vikiisha wanabadilika na kuwa haramu.

Hassan alisema  lengo lao ni kupambana na hali hali hiyo ya uwepo wa wahamiaji haramu ambapo aliomba wakazi wa mkoa wa Pwani kusaidia kwa kutoa taarifa kwenye vyombo husika pindi watakapoona kuna wahamiaji haramu katika maeneo yao.

Alisema wahamiaji haramu wengi wao wanaokamatwa ni wale wanaopita wakielekea maeneo mengine lakini idara ya uhamiaji  wanaendelea kujidhatiti kwa kuziba mianya na maeneo ambayo wakifika wanafanya shughuli nyingine.

Hivi kafibuni wahamiaji Haramu 35 walikamatwa katika eneo la Ubena Zomozi wakiwa wamejificha ndani ya nyumba, hatua za kisheria tayari zimechukuliwa .

No comments:

Post a Comment

Pages