Waziri wa Kilimo Hussein Bashe akifafanua jambo mbele ya wanahabari wakati akielezea mafanikio ya wizara hiyo katika kipindi cha mwaka mmoja ndani ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam
Wizara ya Kilimo imesaini Hati ya Makubaliano ya miaka mitano na Kampuni ya Smart Import and Export ya Misri kwa ajili ya ununuzi wa mahindi ya njano na Rasimu ya makubaliano ya kuiuzia India mazao ya jamii ya mikunde hususan mbaazi imeandaliwa na taratibu zinaendelea.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Kilimo Hussein Bashe wakati akielezea mafanikio ya Wizara hiyo katika kipindi cha mwaka mmoja ndani ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Amebainisha kuwa Serikali imeongeza bajeti ya utafiti kutoka Sh. Bilioni 7.35 hadi Sh. Bilioni 11.63, huduma za ugani kutoka Sh. Milioni 603 hadi Sh. Bilioni 11.5, umwagiliaji Sh. Bilioni 17.7 hadi Sh. Bilioni 51.48, uzalishaji wa mbegu kutoka Sh. Bilioni 5.42 hadi Sh. Bilioni 10.58.
Amesisitiza kuwa Serikali imezipatia NFRA na CPB jumla ya Sh. Bilioni 129 kwa ajili ya ununuzi wa mazao ya nafaka ambayo yatauzwa katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Waziri Bashe ameongeza kuwa wizara hiyo imefanikiwa kufungua masoko mapya ya mazao nje ya nchi ikiwemo soko la Maparachichi (India na Afrika Kusini) na ndizi (Kenya) baada ya kukidhi viwango vya ubora.
“Kumekuwa na changamoto za Utafiti pamoja na soko la uhakika la mazao, mkulima akiwa hana uhakika wa soko inamlazimu kuacha kilimo, Serikali imeangalia ni namna gani tunaweza kutengeneza masoko kwaajili ya kuuza mazao yetu “.Amesema Waziri Bashe.
Amefafanua kuwa CPB imefungua vituo vya mauzo katika miji ya Juba (Sudan Kusini) na Lubumbashi (DR Congo) na kukodi maghala yenye uwezo wa kuhifadhi tani 5,000 na 2,000 mtawalia.
Pia amesema jumla ya Shilingi Bilioni 3.63 zimetolewa kwa ajili ya kuwezesha TARI, TORITA, TRIT, TPHPA na TACRI kuwezesha utafiti wa mazao ya kilimo ikiwemo mchikichi, zabibu, mkonge, ngano, alizeti, kahawa, chai na tumbaku.
Waziri Bashe amesema kuwa miongoni mwa malengo ya Wizara ni pamoja na kuongeza ukuaji wa Sekta ya kilimo kutoka asilimia 5 za sasa kufikia asilimia 10, kuongeza mchango wa Sekta kilimo kwenye GDP kutoka 25% kufikia 35% ifikapo 2030 na kupunguza umaskini kwa zaidi ya asilimia 50 kutoka asilimia 26.4 za sasa kufikia asilimia 13 ifikapo 2030.
No comments:
Post a Comment