Mhandisi Yusufu Juma na Mhandisi Rahel Bulashi wa RUWASA Wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani akichukua kipimo katika ujenzi wa Mradi wa Maji Fukayosi.
Mhandisi Yusufu Juma wa RUWASA Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani akichukua vipimo vya ujenzi wa tekini la maji Mradi wa Maji Fukayosi.
Mkandarasi wa Mradi wa Maji Fukayosi, Mhandisi Mohammed Abdallah, akifafanua kuhusu utekelezaji wa Mradi wa Maji Fukayosi.
Mkandarasi wa Mradi wa Maji kijiji cha Fukayosi, Mhandisi Mohammed Abdallah akifafanua jambo kwa waandishi wa habari kuhusu mradi huo.
Mwananchi wa kijiji cha Fukayosi Pauline akieleza furaha yake baada ya RUWASA kuwapelekea maji.
Na Selemani Msuya,
Bagamoyo
WAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijiji (RUWASA), Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, umetumia Sh.milioni 350 za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19 kuongeza mtandao wa maji kijiji cha Fukayosi.
Fedha hizo ni za mkopo usio na riba wa Sh. trilioni 1.3 kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), ambapo zitawezesha utekelezaji wa Sera ya Maji ambayo inayotaka kila mwananchi kuchota maji mita 400 kutoka nyumbani kwake.
Akizungumza na waandishi wa habari wanaotembelea miradi ya maji inayofadhiliwa na fedha za ustawi Meneja wa RUWASA, Wilaya ya Bagamoyo, Mhandisi James Kionaumela, amesema uamuzi wa kupeleka mradi huo Fukayosi ni kutokana na changamoto ya maji kwa muda mrefu.
Amesema Mradi wa Maji Fukayosi RUWASA umefanyiwa upanuzi kwa kujenga tenki jipya lenye uwezo wa kubeba lita 75,000 za maji na usambazaji wa bomba kilomita 9.2.
Meneja huyo amesema mradi huo ukikamilika utahudumia watu 2,242 ambao walikuwa wanapata maji kwa shida.
Mhandisi Kionaumela amesema upatikanaji wa maji vijiji wilayani Bagamoyo ni asilimia 73 na mijini ni asilimia 84.
Akizungumzia mradi huo, Mkandarasi wa Mradi wa Maji Fukayosi, Mhandisi Mohammed Abdallah, amesema wanatekeleza mradi huo katika ubora na viwango walivyokubaliana na RUWASA.
Mhandisi Abdallah amesema hadi sasa wameshasambaza mabomba ya maji kwa asilimia 90, ujenzi wa vituo vinne na tenki lenye uwezo wa kubeba lita 75,000 lipo katika hatua za mwisho ya ujenzi.
“Nitumia nafasi hii, kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuruhusu wakandarasi wazawa kupewa miradi ya kujenga hatutamuangusha kwa sababu tulipitia wakati mgumu kidogo,” amesema.
Kwa upande wake Mkazi wa Kijiji cha Fukayosi, Salim Hatibu amesema ujio wa mradi huo ni neema ambayo waliisubiri muda mwingi na kuahidi kuutunza.
“Tumekuwa tukiteseka kwa maji kukatika mara kwa mara na wakati mwingine tunakaa siku tatu bila maji. Lakini pia tunanunua maji lita 20 kwa Sh.1,000 sisi wanyonge hatuwezi, hivyo ujio wa mradi huu ni wazi tumekombolewa,” amesema.
Mwenyekiti wa kijiji cha Fukayosi, Rajab Mkecha, amesema kwa muda mrefu wamekuwa na changamoto ya maji katika vitongoji vilivyopo katika kijiji hicho, hivyo wanashukuru kupatiwa mradi huo na RUWASA.
“Vitongoji vya Fukayosi, Umasaini, Chalalabaga na Lusako vilikuwa vinapitia wakati mgumu linapokuja suala la maji. Tunamshukuru Rais Samia ameupiga mwingi katika eneo hili la maji,” amesema.
Naye Mwanamama Semeni Hussein, amesema uamuzi wa RUWASA kuwapelekea maji safi na salama utasaidia afya zao kuwa salama, kwa kuwa watakuwa hawanywi maji pamoja na ng’ombe.
“Tunashukuru ujio wa maji ya uhaki ambayo ni safi na salama, ila tunaomba RUWASA kama wanaweza watukopeshe kwa kutusambazia maji majumbani tulipe kidogo kidogo,” amesema.
Naye Pauline George amesema kinachoendelea kijiji kwao ni utekelezaji wa vitendo dhamira ya Serikali ya kumtua ndoo mama kichwani.
“Sisi kwa miaka mingi tumekunywa maji yenye rangi ya chai ya maziwa, hivyo hiki kinachoendelea tunapongeza sana kwani sasa tutaoga na kunywa maji safi,” amesema.
No comments:
Post a Comment