HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 26, 2022

ZAIDI YA WATOTO 62,155 KUNUFAIKA NA CHANJO YA POLIO IKUNGI


Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Singida Jerry Muro akiongoza kikao cha kuratibu zoezi la Kitaifa la chanjo ya polio kilichofanyika mkoani Singida jana. Kushoto ni Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Winfrida Funto na kulia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Ally Mwanga. 
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo akizungumza kwenye kikao hicho.
Katibu Tawala wa wilaya hiyo Winfrida Funto akizungumza kwenye kikao hicho.
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Oliva Njoka akitoa taarifa kuhusu maandalizi ya chanjo hiyo.
Mwenyekiti wa Halmashauri yaWilaya hiyo Ally Mwanga akizungumza kwenye kikao hicho.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo Mika Likapakapa akichangia jambo kwenye kikao  hicho.
Mratibu wa Elimu ya Afya na Uhamasishaji Wilaya ya Ikungi Braison Shoo akizungumzia ugonjwa huo.
Kikao kikiendelea.
Wajumbe wakiwa kwenye kikao hicho.
Baadhi ya madiwani wa Halmashauri hiyo wakiwa kwenye kikao hicho.


Na Dotto Mwaibale, Ikungi.


MKUU wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Jerry Muro ametoa onyo kwa mtu yeyote wilayani hapa kutokwamisha mchakato wa utoaji wa chanjo ya polio kitaifa utakaoanza Aprili 28 mwaka huu unaotarajiwa kuwafikia watoto 62,155 na atakayebainika akifanya hivyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.

Muro alitoa onyo hilo wakati akizungumza na maafisa mbalimbali, viongozi wa dini, wadau wa maendeleo na timu ya wataalamu watakaoratibu zoezi hilo wilayani hapa ambapo alihamasisha wananchi wote kujitokeza bila kukosa wakati zoezi hilo litakapoanza.

"Sisi hapa Ikungi tupo tayari mpaka sasa  tumepokea jumla ya chanjo 71,400 na tumesambaza dozi 70,000 katika vituo vya kutolea afya na kuwa watalifanya kwenye vijiji vyote 101 na zaidi ya vitongoji 500" alisema Muro.

Alisema tayari wamewapanga wataalamu kwenye vituo 140 na watafika kwenye maeneo yote na kila mtoto aliopo kwenye wilaya hiyo watahakikisha anapata chanjo hiyo.

Muro alisema kwamba miundombinu yote pamoja na timu ya wataalamu kwa ajili ya kuwezesha ufanikishaji wa zoezi hilo yamekamilika kwa asilimia 100.

Aidha Muro alitoa mwito kwa wazazi wilayani humo kuacha tabia ya kuwapeleka watoto wao kwa waganga wa kienyeji kwani hawana uwezo wa kutoa chanjo ya polio badala yake wawapeleke kwenye vituo vya afya wakiwapeleka huko wanaweza kupigwa na ugonjwa  huo na hata kupata kifo.

Muro aliwaomba wazazi hao kuanzia Aprili 28 hadi Mei Mosi kuwa ni kipindi cha mzazi kumpeleka mtoto wake kituo cha afya na yale maeneo yaliopo  pembezoni kabisa mwa wilaya hiyo watayafikia kupitia kampeni ya nyumba kwa nyumba.

 
Muro alitumia nafasi hiyo kupiga marufuku tabia ya wazazi ambao kila wakipewa elimu na kuambiwa umuhimu wa kuwapeleka watoto wao vituo vya afya kwa ajili ya kupewa chanjo wamekuwa mstari wa mbele kukahidi kwa sababu ya imani na mila potofu hivyo kuanzia jana mzazi yeyote watakaye mbaini anakendwa kinyume na maagizo ya kitaifa ya zoezi hilo  atakamatwa na kuchuliwa hatua kali za kisheria na kuwa mfano kwa wengine wote katika wilaya hiyo.

 
"Tumepata taarifa kuwa kuna watu wamejipanga kukwamisha zoezi ili sasa mimi nawaambia kuwa kabla ya kuanza kukwama sisi watakwama wao na waomba watu wote wenye imani potofu dhidi ya chanjo hii watuache kwanza tufanye kazi nipo hapa kwa ajili ya kuwatoa mashaka wananchi wote wa wilaya ya Ikungi kuwa chanjo hizi ni salama zimedhibitishwa na wataalamu wa afya wa kimataifa na hapa nchini" alisema Muro.

 
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ikungi,  Oliva Njoka alisema wamepokea maagizo kutoka wizarani kuwa kunakampeni ya kitaifa ya chanjo hiyo kwa nchi nzima ambapo watachanjwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano na kuwa tayari wamekwisha anza maandalizi kwa kupata mafunzo ngazi ya halmashauri kwa timu ya uendeshaji na pia watatoa mafunzo kwa wale wahudumu watakao kuwa wakichanja.

 
Mratibu wa Elimu ya Afya na Uhamasishaji Wilaya ya Ikungi Braison Shoo alisema hivi sasa wapo kwenye kampeni ambayo wanatarajia kuianza Aprili 28 hadi Mei Mosi ya chanjo ya matone kwa watoto waliochini ya miaka mitano ambapo aliwaomba wananchi wote wa wilaya hiyo kujitokeza kwa wingi kupeleka watoto wao kupata chanjo.

 
Alisema lengo la chanjo hiyo ni kuongeza kinga katika jamii baada ya kutokea mlipuko wa ugonjwa huo nchi jirani ya Malawi hivyo aliendelea kuwasihi wananchi kujitokeza kwa wingi wakati wa zoezi la  chanjo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ally Mwanga na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo,  Mika Likapakapa walisema watakwenda kuwahimiza madiwani na viongozi wa chama na serikali ngazi za vijiji na kata kwa ajili ya kuhamasisha zoezi hilo ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.


No comments:

Post a Comment

Pages