HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 10, 2022

UNCDF yawabeba wabunifu Tanzania

Mkurugenzi wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dk. Amos Nungu akizungumza wakati wa kongamano la waandishi wa habari Dar es Salaam.
Baadhi ya wawakilishi wa waandishi wa habari waliohudhuria kongamano hilo wakijadili masuala mbalimbali yanayoweza kuzitangaza bunifu za watanzania nje ya nchi.

Na Mwandishi Wetu

MFUKO wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya Mitaji (UNCDF), umeahidi kuendelea kufadhili kazi bunifu za vijana wa Tanzania kwa fedha na huduma za kitaalam ili kukuza na kiendeleza bunifu hizo.

Ahadi hiyo imetolewa na Mwakilishi wa UNCDF, Paul Damocha, wakati wa kongamano la waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana ikiwa ni maadhimisho ya matukio mbalimbali kuelekea wiki ya ubunifu Tanzania itakayoanza Mei 16 hadi Mei 20.2022.

Alisema mfuko huo kwa kushirikiana na serikali wametengeneza miongozo mbalimbali ya kuwasaidia wabunifu kuleta bunifu zitakazotoa majibu ya matatizo yaliyopo katika jamii na kuthibiti kazi hizo ili ziwe zenye manufaa.

‘’Tutahakikisha wabunifu wote ambao bunifu zao zimetambuliwa na serikali wanapatiwa fedha na msaada wa kitaalamu ili kubuni vitu vingi zaidi na kuajiri watu wengine,’’ alisema Damocha.

Awali Mkurugenzi wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dk Amos Nungu, aliwaeleza waandishi wa habari kwamba Serikali ina nia njema ya kuwakuza na kuwatangaza wabunifu wadogo huku ikiwahakikishia usalama wa watumiaji wa bunifu zao.

Kwa mujibu wa Dk. Nungu, serikali inaendelea kuwatambua na kuwaendeleza wabunifu ambao wamejiajiri ili kutengeneza bidhaa salama za kurahisisha maisha ya watu.

“Wiki ya Ubunifu Tanzania imeandaliwa na Mradi wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) kupitia mradi wa Funguo kwa kushirikiana na COSTECH, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia  na wadau wa sekta ya mawasiliano.

‘’Jukumu la serikali ni kulinda usalama wa watu wake. Kumekuwa na malalamiko mengi kuwa vijana wadogo wabunifu wamezuiwa kuendeleza kazi zao  si kweli, kwa mfano kuna kijana kule Mbeya ambaye alibuni helikopta nilifika nikaiona lakini ni lazima tujihakikishie usalama wa abiria kama inaweza kuruka kulingana na viwango vya kimataifa na abiria watakuwa salama,’’ alisema Dk. Nungu.

Aliongeza kuwa wabunifu wamefanikiwa kujiajiri na kuajiri watu wengine kwa kuuza bunifu zao na kuliingizia taifa fedha ambazo zinachangia katika ukuaji wa uchumi.

‘’Kutakuwa na Wiki ya Ubunifu ambayo itaanza Mei 16 hadi 20, mwaka huu katika Mikoa 16 ikiwemo Dar es Salaam, Dodoma, Zanzibar, Mbeya na Morogoro ili kuona kazi za kibunifu zilizofanywa na vijana wetu zitakazosaidia kutatua changamoto katika jamii,’’ alisisitiza.

Mtaalamu wa Miradi wa UNDP, Emmanuel Nnko alisema ubunifu ni nyenzo muhimu katika kusukuma mbele maendeleo katika sekta mbalimbali.

No comments:

Post a Comment

Pages