Katibu wa Chama cha Wasioona (TLB) Kagera wilayani Misenyi Godfrey Salvatory.
Na Lydia Lugakila, Kagera
Ushirikishwaji haba katika miradi mbalimbali ya kimaendeleo yatajwa kuwabagua na kuwanyima fursa watu wenye ulemavu.
Hayo yamebainika katika ziara ya kuwatembelea watoto wenye ulemavu wilayani Misenyi Mkoani Kagera.
Akizungumzia hali hiyo Katibu wa Chama cha Wasioona TLB Kagera wilayani Misenyi, Godfrey Salvatory, amesema suala la elimu juu ya watu wenye ulemavu haitoshi kwani baadhi ya viongozi toka ngazi ya chini hawawathamini licha ya serikali kuu kuweka juhudi katika kuwatambua na kuwajali katika miradi mbali mbali ya kimaendeleo.
"Ubaguzi mkubwa umekuwepo upande wa miradi ya serikali kwani serikali kuu inasema sisi wenye ulemavu tushirikishwe katika miradi yote ila baadhi ya viongozi wa ngazi za chini wanaopewa maagizo ufanya ubaguzi kwa kweli tunabaguliwa"alisema Salvatory.
Akichukulia mfano wa eneo lililowabagua, Salvatory amesema ni katika mradi wa TASAF ambapo wamekuwa hawashirikishwi kabisa ambapo wanaoingizwa katika mradi huo wengi ni wenye kipato huku wao wakiachwa nyuma na wanapojaribu kuhoji huambiwa watu wenye ulemavu ni wasumbufu.
Aidha katibu huyo ameipongeza wilaya ya Misenyi inavyowajali watu wenye ulemavu na kuiomba serikali kuu kuwahimiza viongozi ngazi ya chini kuwashirikisha watu wenye ulemavu ipasavyo katika miradi mbali mbali ili kuondoa unyanyapaa.
Hata hivyo ziara ya kuwatembelea watoto wenye uoni hafifu imemuibua Jakline Jofrey mwenye umri wa miaka 18 mwanafunzi wa kidato cha tatu shule ya sekondari Bwanjai na Jonson Jofrey mwanafunzi wa darasa la tano shule ya msingi Mugana ambapo wameomba kusaidiwa kupata matibabu ya macho kwani hata wanapokuwa wakifanya mitihani yao darasani huchelewa kumaliza hadi waongezewe muda.
Kwa upande wao walimu wa watoto hao akiwemo mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mugana B Bi Grace Nkwama na mkuu wa shule ya sekondari Bwanjai wameipongeza chama cha wasioona TLB Kagera kwa juhudi wanazofanya kwa kushirikiana na wadau mbali mbali katika kuwaibua na kuwatambua watu wenye ulemavu mkoani humo huku wakiwashauri wazazi kutoficha kasoro za watoto badala yake watoe mara watoto wanapopelekwa shule ili kuona namna nzuri ya kuwahudumia sawa na watoto wasio na ulemavu.
No comments:
Post a Comment