Na Mwandishi Wetu
KIONGOZI wa Mbio za Mwwnge wa Uhuru kitaifa 2022, Sahil Geraruma amewataka viongozi wilayani Korogwe kununua kuku na mayai kutoka shamba la ufugaji la Nyakusagila One Poultry Farm pindi wanapopata ugeni wlayani humo.
Geraruma ametoa kauli hiyo leo Jumapili Juni 5, 2022 wakati Mwenge wa Uhuru ulipotembelea mradi huo unaoendeshwa na mwekezaji mzawa wilayani humo.
“Binafsi nimefurahishwa na mradi huu nawasihi viongozi mnapopata ugeni mbalimbali kama huu wetu mnunue kutoka kwake ili kumuunga mkono na uongeza ajira kwa vijana wetu,” amesema.
Awali akisoma taarifa ya mradi huo, Meneja Mradi Steven Bendera amesema mradi huo umekuwa na manufaa kwao na jamii kwa kuwa unatoa fursa kwa wananchi na taasisi mbalimbali kuja kujifunza dhana ya ufugaji kuku wa kisasa ambapo wamekuwa tayari kutoa elimu pale inapohitajika.
Amesema mradi huo ulianza kwa mwaka 2021 ambapo awamu ya kwanza ya majaribio walianza kwa kununua vifaranga 2,500 kutoka Kampuni ya kuzalisha vifaranga ya Interchick na kufikia leo kuwa na kuku 1,625 ambao wanaendelea kutaga na kuzalisha wastani wa trei za mayai 41-47 kwa siku sawa na asilimia 75.
“Lengo la mradi wetu ni kuzalisha mayai bora ya kisasa ili kukidhi mahitaji ya watumiaji ndani ya Wilaya ya Korogwe na hivyo tumedhamiria kwa kipindi cha miaka miwili tangu kuanzishwa kwa mradi huu tuwe na kuku 10,000 na kuwa na kuku 20,000 katka malengo yetu ya muda mrefu kwa kuongeza miundombinu ya kubeba kuku wote.
“Mradi huu umeajiri msimamizi mmoja ambaye chini yake ana vibarua wa siku watatu na kufanya jumla kuwa na wafanyakazi wanne,” amesema.
Pamoja na mambo mengine, Mwenge wa Uhuru leo umefikisha siku ya 10 mkoani Tanga ambapo utakuwa wilayani Korogwe katika miradi ya Halmshauri ya Mji Korogwe utakapohitimisha mbio hizo kabla ya kesho kukabidhiwa kwa Mkoa wa Kilimanjaro.
No comments:
Post a Comment