HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 21, 2022

OFISI YA WAKILI MKUU WA SERIKALI YAANZA UJENZI WA OFISI KATIKA MJI WA SERIKALI MTUMBA, DODOMA

 

 Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende (aliyesimama katikati) akiwa na wawakilishi wa Kampuni ya Ujenzi ya SUMA JKT na TBA pamoja na baadhi ya watumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali baada ya hafla fupi ya kukabidhi eneo la ujenzi wa jengo la makao makuu ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali lililopo Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma.

 

 Na Prisca Ulomi, OWMS

Wawakilishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS) wakiongozwa na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende leo tarehe 18 Juni, 2022 wameshuhudia makabidhiano ya eneo la ujenzi wa Ofisi za Makao Makuu ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali lenye  ukubwa wa mita za mraba 17,342. Makabidhiano hayo yamefanyika kwenye Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma baina ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ambaye ni Mshauri Elekezi aliyewakilishwa na Msanifu Majengo Weja Ng’olo na Kampuni ya Ujenzi ya SUMA JKT ambae ni Mkandarasi iliyowakilishwa na Mkadiriaji Majenzi, Jacob Ghati.

Akikabidhi eneo hilo, Mwakilishi wa TBA, Ng’olo ameeleza kuwa jengo la Ofisi linalotarajiwa kujengwa ni la kisasa na ni miongoni mwa majengo yenye muonekano mzuri katika Mji wa Serikali Mtumba. Jengo hili litakuwa na miundombinu mbalimbali ikiwemo vyumba vya Ofisi 127, maegesho ya magari 111, maktaba, kumbi 2 za mikutano zenye nafasi 108 kila mmoja, kumbi 2 za kutolea mafunzo zenye nafasi 42 kila mmoja, maabara ya kompyuta, vyumba vidogo 10 vya mikutano na chumba cha akina mama wanyonyeshao. Ujenzi wa jengo hilo unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi kumi na nane (18).

Akizungumza kwa niaba ya Mkandarasi, Gati amesema kuwa wako tayari kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa mujibu wa mkataba na kwa kushirikiana na Mshauri Elekezi (TBA) na Mshitiri (OWMS).

Kwa upande wake, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Luhende amewatakia Mkandarasi na Mshauri Elekezi utekelezaji mwema wa majukumu yao kwa mujibu wa mkataba na kwa kuzingatia weledi. Pia amewahakikishia kuwa Ofisi ya Wakili Mkuu Serikali itawapa ushirikiano unaostahili.

No comments:

Post a Comment

Pages