HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 03, 2022

RAIS SAMIA AZITAKA HALMASHAURI ZA WILAYA KUIGA UFANYAJI KAZI WA TASAF

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan (katikati) akiwa na viongozi mbalimbali wakati akikata utepe kuashiria kukabidhi magari 123 yenye thamani ya  Sh. 10.48 Bilioni kati ya 241 yaliyotolewa na Serikali kwa Mamlaka za maeneo ya utekelezaji kwa shughuli za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa Tanzania Bara na Zanzibar katika hafla iliyofanyika katika Viwanja vya Posta, Kijitonyama Jijini Dar es Salaam jana.

Mnufaika wa TASAF Khadija kutoka Kikundi cha Kwa Raha Zetu akimuonesha Rais Samia Suluhu Hassan bidhaa anazozitengeneza alipotembelea mabanda ya wanufaika.
 Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Ladislaus Mwamanga akitoa taarifa ya utekelezaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) 
Wakuu wa Wilaya za Dar es Salaam wakiwa kwenye hafla hiyo.
Rais Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali.
Rais Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na Wafanyakazi wa TASAF.
Baadhi ya viongozi waliokabidhiwa magari hayo kwaniaba ya wenzao wakionesha mfano wa funguo baada ya kukabidhiwa na Rais Samia Suluhu Hassan. Kutoka kushoto ni Katibu Tawala Mkoa wa Njombe,  Judica Omari. Mkurugenzi Idara ya Uratibu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Siajabu Pandu na Profesa Faustine Kamuzora.
Wananchi na wadau wangine wakiwa kwenye hafla hiyo.
Muonekano wa sehemu ya magari yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kutekeleza miradi ya TASAF.
Magari yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya TASAF.
Sehemu ya magari yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kutekeleza miradi ya TASAF.
Baadhi ya wanufaika wa TASAF wakiwa kwenye mabanda yao wakimsubiri Rais Samia Suluhu kuyatembelea.
 

Na Dotto Mwaibale, Dar es Salaam


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan Hassan amezitaka Halmashauri za wilaya kote nchini kuiga mfano wa utendaji kazi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF)

Kauli hiyo imetolewa na Rais Samia wakati akizungumza na viongozi mbalimbali pamoja na wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam kabla ya kukabidhi magari 123 yenye thamani ya Sh.10.48 Bilioni kati ya 241 kwa Mamlaka za maeneo ya utekelezaji kwa shughuli TASAF kwa Tanzania Bara na Zanzibar katika hafla iliyofanyika Viwanja vya Posta, Kijitonyama Jijini Dar es Salaam jana..

“Mifumo mizuri ya ufanyaji kazi wa TASAF ndio iliyofanikisha mpango huu wa Kipindi cha Pili Awamu ya Tatu kuwa na mafanikio hivyo ni vizuri ukaendelea ” alisema Rais Samia Suluhu Hassan.

Katika hatua nyingine Rais Samia Suluhu Hassan ameomba viongozi wa ngazi za chini ambao wanaratibu mpango wa TASAF ili hali nao maisha yao ni ya chini waingizwe kwenye mpango huo ili nao wawe wanufaika kwani mpango huo upo kwa ajili ya kuwainua wananchi wote.

Aliwataka TASAF kusimamia vizuri fedha hizo na kuwa kuna watu wapo midomo wazi na wanafanya kila wanavyoweza wale fedha hizo na inapotokea mtu mmoja akaonekana mgumu katika kuziachia fedha hizo zisiliwe ndio atapigwa vita hivyo aliwasihii watendaji hao wachukue kile kinachowapasa kupata kutokana na kazi yao na wasichukue mali ya wanyonge .

Alisema TASAF wamefanya vizuri na lengo kubwa la mpango huo ni kuwatoa wananchi kwenye mazingira magumu na akawasisitizia kuwa mbali ya kazi hiyo nzuri wanaoifanya wafanye kazi ya kutoa elimu kwa ajili ya kuwatoa kwenye umasikini wa  fikra na kuishi maisha yanayoelekea akitolea mfano kuwa kuna watu wanang’ombe wengi lakini ukiangalia nyumba wanayoishi hailingani na utajiri walionao na kiafya sio nzuri.

Aidha Rais Samia Suluhu akitoa maagizo kuhusu matumizi ya magari hayo ambayo yamepatikana kwa mkopo alisema yanatakiwa kutunzwa huku akisisitiza kauli ya msanii wa mashairi Farida Rajabu aliyeimba akisema magari hayo yasiende kutumika kwa ajili ya kubebea mkaa na kuni bali yafanye kazi iliyokusudiwa ya kutembelea na kukagua miradi yote inayotekelezwa na TASAF kama ilivyoahinishwa kwenye mkataba.

Alisema magari hayo yatawekewa mfumo utakaowezesha kuonekana wakati wote na shughuli yanayoifanya.

“Mfumo huo utaonesha mwenendo wa gari husika mahali lilipo na lipo kwa shughuli gani lengo likiwa i kuangalia matumizi na usalama wake na kuwa watafunga mfumo huo kama wanavyofanya wamiliki wa magari binafsi wanavyofanya kwenye magari yao ya biashara” alisema Rais Samia.

Alisema magari hayo wakati wote yatakapo kuwa kazini yatakuwa chini ya uangalizi wa wakurugenzi wa halmashauri za wilaya inapotekelezwa miradi mbalimbali ya TASAF.

“Magari nitakayokabidhi ni 123 lakini fedha nilioitoa Serikalini ni ya magari 241, magari haya yote yatanunuliwa kwa ajili ya TASAF katika  Halmashauri zote 184, makao makuu ya TASAF lakini pia TAMISEMI nao watapata” alisema Rais Samia. 

Pia Rais Samia Suluhu Hassan alipendekeza magari hayo kufanyiwa matengenezo na Kampuni ya TOYOTA ambayo imewauzia na akaagiza magari yote ya awali yaliyokuwa yakitumika katika mpango huo wa TASAF yarudishwe Makao Makuu ya TASAF  jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia utekelezaji wa TASAF Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Ladislaus Mwamanga alisema Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ulianzishwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2000 kwa ushirikiano na wadau mbalimbali wa Maendeleo katika jitihada za kupunguza umaskini kwa kutumia dhana ya ushirikishwaji Jamii.

Alisema Programu ya TASAF imetekelezwa katika Awamu Tatu na imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali katika ngazi ya Jamii kwa lengo la kupunguza umaskini kwa msingi wa kutoa huduma za jamii katika sekta zote. 

Alisema utekelezaji huo umekuwa ukizingatia mahitaji halisi au kero za wananchi wenyewe kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Serikali. 

Mwamanga alisema kuanzishwa kwa TASAF na utekelezaji wake katika Awamu zote Tatu kunatokana na umuhimu ambao serikali imeuweka katika kutekeleza sera na mikakati yake ili kuwajumuisha wananchi wote katika kujenga uchumi imara na kuleta maendeleo kwa wote. 

Alisema kimsingi utekelezaji wa TASAF Kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu unachangia kufikia malengo kama yalivyoainishwa katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22-2025/26) ili kuhakikisha ushiriki wa watu katika kujenga uchumi jumuishi (inclusive economic growth) kwa kushiriki kwenye mikakati ya kupunguza umaskini na kujega Rasilimali Watu na kuongeza uwezo wa kiuchumi kwa vijana, wanawake na wenye ulemavu. 

Mwamanga alisema ili hayo yaweze kufanikiwa, TASAF imejenga ushirikiano mzuri na Mamlaka za Utekelezaji ambapo kwa Pamoja tumefaulu kutekeleza Mpango huu kwa ufanisi na kuwa ushirikiano huo umeijengea heshima nchi yetu kwani kupitia Mipango mbalimbali ya Serikali na Mpango huo wa TASAF Tanzania inashika nafasi ya Kwanza kwa Afrika na nafasi ya Pili Duniani kwa kujenga uchumi jumuishi. 

Alisema jambo hilo limewezekana kutokana na ushirikiano uliopo katika ngazi zote za utekelezaji. 

" Nitoe shukurani za dhati kwa Viongozi wa Mamlaka zote za Utekelezaji na Ufuatiliaji kwa juhudi kubwa wanazofanya kufanikisha utekelezaji pia  tunaishukuru Serikali yetu ya Awamu ya Sita  chini ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza utekelezaji wa shughuli za TASAF na  kuithinisha kuandikisha  kaya mpya 498,091 kwenye Mpango wa TASAF ili ziweze kushiriki katika shughuli za Kukuza Uchumi wa Kaya  na pia kutoa fedha za Uviko -19 Sh. Bilioni 5.5 ile ziweze kuwafikia  walengwa wa TASAF katika maeneo yaliyo hatarishi kwa ugonjwa wa Uviko - 19" alisema Mwamanga. 

Alisema Awamu ya Tatu ya TASAF Kipindi cha Pili ndiyo inayotekelezwa sasa. Utekelezaji wa Awamu hiyo ulianza Februari 2020 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2025 na kuwa kipindi hicho cha Pili cha Awamu ya Tatu kimetengewa fedha Sh. Trioni 2.0. 

Alisema katika utekelezaji wa kipindi hicho cha Pili mambo mengi yamefanyika yenye mafanikio ambayo ni pamoja na    Uhakiki wa awali wa Kaya katika Mamlaka 186 za utekelezaji ambapo jumla ya Kaya 886,724 zilihakikiwa na kaya 781,342 zimekidhi vigezo vya uhakiki wa awali wa kuendelea kuwepo katika Kipindi cha Pili cha Mpango na kaya 105,382 zimeboreka kiuchumi na kupewa muda wa kujiandaa ili kutoka kwenye mpango na kujitegemea kiuchumi.

Alitaja mafanikio mengine kuwa ni utambuzi na uandikishaji wa kaya maskini kwa Vijiji/Mitaa/Shehia ambazo hazikufikiwa na Mpango wa Kipindi cha Kwanza umefanyika na umekamilika katika Mamlaka zote 186 ambapo Mitaa/Vijiji/Shehia 7,217 vimefikiwa na jumla ya Kaya mpya 498,091 ziliandikishwa na hivyo kufanya Mpango kuwa na Kaya za Walengwa 1,279,325 zenye zaidi ya watu Milioni Sita, Ruzuku ya Sh.Bilioni 266 ilihawilishwa kwa kaya 1,279,325 zilizokidhi vigezo vya kuingia katika Kipindi cha Pili cha Mpango kutoka maeneo yote ya utekelezaji 184 kwa Tanzania Bara na Pemba na Unguja kwa Zanzibar,      Miradi 2,674 ya Kutoa Ajira za Muda kutoka katika mamlaka za utekelezaji 51 imeibuliwa na jamii. 

Aidha Mwamanga alisema miradi hiyo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na inatoa Ajira ya Muda kwa kaya 253,117. 

Alisema hadi kufikiaMei 2022, jumla ya Sh.Bilioni 25.14 zimeshalipwa kwa walengwa kama Ujira. Pia mafunzo ya usimamizi wa miradi yamefanyika kwa wawezeshaji 1,399 kutoka mamlaka 51 za utekelezaji zinazotekeleza miradi kwa mwaka wa fedha 2021/2022, miradi 550 ya miundombinu imeandaliwa na kutekelezwa ambapo miradi mitatu kati ya hiyo yenye thamani ya Sh. Milioni 321.21 imekamilika wakati mingine 547 yenye thamani ya Sh. Bilioni 16.0 ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. 

Alisema miradi hiyo itawezesha upatikanaji wa huduma za elimu, afya, maji, mazingira, barabara za vijijini na miradi ya ujasiriamali kwa wananchi wanaoishi maeneo husika. 

Aidha Mwamanga alisema jumla ya wataalam 120 kutoka mamlaka 44 za utekelezaji wamepatiwa mafunzo ya uwezeshaji na usimamizi wa miradi, jumla ya Vikundi 30,648 vya Kuweka Akiba na Kuwekeza vimeundwa vyenye wanachama  421,353. na kuwa vikundi hivi vinafanya shughuli  mbalimbali za Ujasiriamali na Wanachama wake wamejiwekea Akiba ya Sh.Bilioni 6.0 na kati ya hizo wamekopeshana Sh.Bilioni 2.9 ili kuweza kuanzisha au kuendeleza miradi ya kuongeza kipato. 

Alisema vile vile kiasi cha Sh. Bilioni 2.25 zimetolewa kama ruzuku kwa vikundi kwa walengwa 4,884 wa mamlaka za utekelezaji za Bagamoyo na Chalinze kwa ajili ya miradi ya ujasiriamali kwa lengo la kukuza Uchumi wa Kaya zao. 

Alisema katika kuimarisha Rasilimali watu, ikiwa ni mkakati moja wapo wa Mpango, mwaka 2019 walipata wanafunzi 277 toka kaya za Walengwa,  mwaka 2020 tulipata wanafunzi 782 toka kaya za walengwa na  mwaka 2021 walipata wanafunzi 1,200 toka kaya za Walengwa waliomaliza kidato cha sita na  walipata Mkopo asilimia 100 kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ( HESLB) na kujiunga na Vyuo Vikuu mbali mbali nchini. 

Mwamanga alitumia nafasi hiyo kuwapongeza Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi ya Elimu ya juu kwa kutoa ushirikiano huo na kuwa wana hati ya makubaliano. 

Halikadharika Mwamanga alisema kwa kutambua kuwa  wanafunzi wanaomaliza Darasa la Saba, Kidatu cha Nne na Kidato cha Sita kutoka Kaya za Walengwa ambao wanakosa nafasi ya kuendelea kimasomo  TASAF inashirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu  kuwapatia Vijana hao Mafunzo ya kuongeza ujuzi mbalimbali Kupitia Programu ya Taifa ya Ukuzaji Ujuzi. 

Alisema idadi ya mamlaka za utekelezaji zilizoingizwa katika malipo ya njia ya Kielektroniki imeongezewa hadi kufikia mamlaka za utekelezaji 122 na kuwa njia hiyo ya malipo inawezesha fedha kutumwa moja kwa moja kwa mlengwa kupitia mitandao ya simu, Benki kwa namba ya NIDA na kumfikia kwa haraka na kupunguza gharama za uendeshaji; lengo ni kuzifikia Halmashauri zote ifikapo June 2022. 

Aidha Mwamanga alisema walengwa kwa kutumia Ruzuku na Ujira walioupata kutokana na Mpango, Walengwa hao wameweza kuboresha maisha yao kwa kuanzisha shughuli za kujipatia kipato na kuwekeza kwenye shughuli za kichumi na Baathist kwa kaya Kaya 27,175 zinafuga ng’ombe 51,299, Kaya 150,043 zinafuga na kumiliki mbuzi 2,745,000,Kaya 38,431 zinafuga na kumiliki nguruwe 781,400, Kaya 40,066 zinafuga na kumiliki kondoo 193,608,Kaya 562,934 zinajishughulisha na miradi ya kilimo,Kaya 33,613 zinajishughulisha na uvuvi, Kaya 210,755 zimeanzisha biashara ndogondogo ili kuongeza kipato cha kaya,Kaya 183,239 zimeweza kuboresha nyumba zao kwa kujenga upya au kukarabati nyumba zao na  Kaya 172,738 zilinunua mabati 1,802,285 ili kuweza kuezeka nyumba zao walizokuwa wamejenga. 

Mwamanga alisema TASAF wanaendeleza ushirikiano katika ngazi zote za utekelezaji na tunawaomba Viongozi kuwatembelea Walengwa na kuona shughuli zao mbalimbali zinazochangiwa na TASAF. Utaratibu huu utasaidia kuwajengea imani wananchi kuona matatizo yao yanawafikia Viongozi, yanasikilizwa na kushughulikiwa. 

Mwamanga alitumia nafasi hiyo kuiomba Serikali kuendelea kuiangalia vizuri TASAF na kuendelea kuipatia Fedha za kutosha ili kutimiza malengo ya Mpango  ipasavyo.

No comments:

Post a Comment

Pages