Mwendesha Mafunzo ya Wajasiriamali Wanawake Dk. Victoria Kisyombe (kushoto), Balozi wa Marekani nchini Dk. Donald Wright (wa pili kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri, wakipozi kwa picha wakati wa kumkabidhi cheti cha kuhitimu mafunzo hayo, Aslatu Nguku, ambaye ni miongoni mwa wajasiriamali 31 kutoka Dodoma waliokamilisha mafunzo hayo.
Dodoma – Wajasiriamali wanawake 31 kutoka Dodoma, leo wamehitimisha mafunzo maalumu ya wiki 10 katika biashara na ujasiriamali yaliyofadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia kupitia programu yake ya kuwajengea uwezo wajasiriamali wanawake (Academy of Women Entrepreneurs – AWE).
Katika mahafali yao yaliyohudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Jabir Shekimweri na wageni wengine waalikwa, wanawake hawa wajasiriamali walipongezwa kwa kuhitimu mafunzo yao na kuhimizwa kuendelea na kuboresha shughuli zao za uzalishaji mali na kujiongezea kipato. Serikali ya Marekani iliwakilishwa na Balozi wa Marekani nchini, Balozi Donald Wright.
AWE ni mpango wa Kimataifa wa Serikali ya Marekani wa kuwawezesha wanawake kiuchumi unaokusudia kuwajengea uwezo wanawake milioni 50 duniani kote kufikia upeo wa uwezo wao kiuchumi. AWE ina dhamira ya dhati ya kuwapa wanawake elimu na ujuzi, kuwajengea mitandao na kufungua fursa wanazohitaji ili kuyabadilisha mawazo yao kuwa miradi halisi ya kujiletea kipato.
Akizungumza na wahitimu katika mahafali hayo, Balozi Wright alielezea matokeo ya mafunzo yanayotolewa na AWE. “Mafunzo ya wiki 10 mliyoyapata mkiwa sehemu ya programu hii yamewapa ujuzi kwa vitendo utakaowawezesha kuanzisha biashara endelevu pamoja na kuwaunganisha na wakufunzi (mentors) na wajasiriamali kama ninyi wa nchini Marekani,” alisema.
Aliendelea kusema kuwa kuwajengea wanawake uwezo wa kiuchumi ndio njia ya haraka zaidi ya kuibadilisha jamii. “Jitihada za wanawake huwa na matokeo makubwa zaidi kwa jamii nzima kwa sababu wanawake wanapofanikiwa mara nyingi watawekeza mapato yao katika familia na jamii zao, wakigharamia mahitaji kama vile ada kwa watoto wao na huduma za afya. Manufaa ya kiuchumi ya mafanikio yenu yanasaidia vizazi vijavyo. Tayari ubunifu wenu unaleta matokeo chanya katika jamii na uchumi wa Tanzania,” alisema.
Wakati wa mahafali hayo, Balozi Wright alitangaza ufadhili za ziada wa Dola za Kimarekani 100,000 kwa ajili ya programu ya AWE nchini Tanzania.
Kundi la wahitimu wa Mwanza ni kundi la tano la washiriki wa programu ya AWE. Kundi la kwanza la wanawake 20 lilihitimu tarehe 9 Septemba, 2019 jijini Dar es Salaam. Kundi la pili lililokuwa na wanawake wajasiriamali 25 kutoka Iringa lilihitimu tarehe 16 Desemba 2020. Kundi la tatu lililokuwa na washiriki 17 kutoka Zanzibar lilihitimu tarehe 28 Juni 2021. Kundi la nne lililokuwa na washiriki 32 kutoka Mwanza, lilihitimu tarehe 8 Novemba 2021.
Kupitia Ubia na Taasisi ya Marekani ya Maendeleo ya Afrika (U.S. African Development Foundation -USADF), wajasiriamali wanaoshiriki programu ya AWE wanaweza kupatiwa na USADF fedha za mtaji wa hadi Dola za Kimarekani 25,000 ili kupanua biashara zao.
Ubalozi wa Marekani unashirikiana na Selfina kutekeleza programu ya AWE nchini Tanzania. Ikiwa imeanzishwa mwaka 2002 na Dk. Victoria Kisyombe, Selfina ni taasisi ya Kitanzania ya utoaji mikopo midogo midogo iliwalenga zaidi akina mama wajane na wasichana. Katika miaka 19 iliyopita, Selfina imewawezesha kiuchumi zaidi ya wanawake 31,000 kupitia mikopo inayozunguka. Maisha ya zaidi ya watu 300,000 yamegushwa kutokana na faida zilizopatikana kutokana na mikopo hiyo. Wanawake sasa ni wamiliki wa biashara zao wenyewe na zaidi ya nafasi za ajira 150,000 zimetengenezwa.
No comments:
Post a Comment