Mauwa Mohammed Mussa Zanzibar
CHAMA cha ACT-Wazalendo kimehoji juu ya kitendo cha Serikali ya Zanzibar kuuza nyumba za serikali za Mji mkongwe kwa kukosa uwazi na uadilifu.
Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Kiongozi Mkuu wa chama hicho, Ismail Jusa Ladhu, wakati akizungumza na wandishi wa habari katika ofisi ya chama hicho iliopo Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar.
Jusa alisema ingawa awali yalitolewa matangazo ya kukaribisha ununuzi lakini baada ya hapo kila kitu kimekuwa cha siri na kupelekea masuala mengi yanayohitaji majibu ikiwemo ni watu wangapi walioomba kununua nyuma hizo na bei iliyotolewa na kila mmoja.
Pili ni vigezo gani vilivyotumika katika kuwabariki waliouziwa nyumba hizo na kiasi gani cha fedha kilichopatikana na ni vipi maslahi ya umma yamezingatiwa.
“Ni muhimu kupata majibu ya masuali hayo kwa vile zipo hoja kwamba baadhi ya nyumba wameuziwa watu ambao hawakuomba kuuziwa”alisema Jusa.
Aidha alisema nyumba ambayo ikimilikiwa na shirika la nyumba waliouziwa mwanzo walipewa kwa bei ya chini sana na wala haijulikani ni kwa vigezo gani, baadae walipokonywa na serikali kwa kisingizio kuwa wamepewa kwa bahati mbaya na kuuziwa mtu ambae hakuomba na haijulikani kwa kiasi gani.
Sambamba na hilo Jusa alisema katika jambo hili la nyumba za mji Mkongwe jambo ambali limezua masuala makubwa na kuwashangaza wananchi wengi ni lililohusu skuli ya Tumekuja ambayo ni skuli yenye historia kubwa kwa Zanzibar.
Alisema skuli hiyo imetangaziwa kupewa mwekezaji kwa hoja za kuwa ni mbovu na hatari kwa wanafunzi ambapo wanafunzi wameonekana wakihamishwa na madeks yao ya kukalia.
“Baada yake tumeambiwa mwekezaji aliyepewa skuli hiyo atajenga madaraza 40 katika eneo la Mwembeladu hatujui kutofautisha thamani ya eneo kama Shangani linalokabiliana na bahari (prime location ) na eneo kama la Mwembeladu”. alisema Jusa.
Hata hivyo alihoji kuwa serikali imeshindwa kuwa na pesa za kulitengeneza na kulitunza jengo hilo la skuli ya Tumekuja skuli ya historia kwa Zanzibar hivyo maeneo ya uekezaji yamemalizika hadi tutoe skuli kugeuzwa hoteli ? alihoji.
Hata hivyo alisema iwapo mwekezaji huyo ana mapenzi makubwa na Zanzibar ni kwa nini asitengeneza skuli ya Tumekuja na kuwakabidhi serikali ili iendelee kutumika kama skuli.
Aidha Jusa alisema chama chake kitasimamia urithi wa kitaifa ili kutekeleza waajibu wao wa kikatiba kama ambavyo wananchi wa Zanzibar wanakitegemea kisimamie hoja zao.
No comments:
Post a Comment