Afisa Mwandamizi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, Eline Maronga akitoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali kwa wateja mbalimbali waliotembelea Banda la HESLB wakati wa maonesho ya 17 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia (HESTE) yaliyoandaliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania TCU yanayoendelea katika Viwanja vya Mnazimmoja Jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
Serikali imesema imetumia kiasi cha TZS 5.3 Trilioni kwa ajili ya kulipa mikopo ya wanafunzi waliojiunga na masomo ya elimu ya juu nchini kati ya mwaka 2005/06 hadi mwaka 2021/2022.
Hayo yamesemwa leo (Jumanne Julai 19, 2022) na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa wakati wa uzinduzi wa maonesho ya 17 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia (HESTE) yanayoendelea yaliyoanza Julai 18-23 Julai katika Viwanja vya Mnazimmoja Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Majaliwa amesema malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuhakikisha kuwa wanafunzi wahitaji wanapatiwa mikopo ya elimu ya juu na hatimaye kuweza kutoa mchango katika ukuaji wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.
“Serikali imekuwa ikiongea kiwango cha bajeti ya mikopo mwaka hadi mwaka, mathalani mwaka 2021/2022 bajeti ya mikopo ya elimu ilikuwa TZS 570 Bilioni iliyonufaisha wanafunzi 177,343 wakiwemo wanafunzi 70,000 wa mwaka wa kwanza” amesema Majaliwa.
Aidha Mhe. Majaliwa amesema malengo ya Serikali ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2025/2026 kutoa mikopo kwa wanafunzi 400,000 ili kuweza kupanua wigo mpana zaidi kwa wanafunzi wahitaji kuweza kupata mikopo ya elimu ya juu.
Mhe. Majaliwa pia aliipongeza Benki ya NMB kwa kutenga kiasi cha TZS 200 Bilioni kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wanaotarajia kujiunga na masomo ya elimu ya juu kwa mwaka 2021/2022 na kuzitaka taasisi nyingine kuiga mfano huo.
Maonesho ya HESTE 2022 yaliyoandaliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) yana kauli mbiu isemayo “Elimu ya Juu inayokidhi mahitaji ya soko la Ajira kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi”.
No comments:
Post a Comment