HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 31, 2022

TMDA yaanzisha mfumo wa kielektroniki katika kutoa taarifa

 


 

Na Jasmine Shamwepu, Dodoma


MKURUGENZI Mkuu Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Adam Fimbo amesema kwa mwaka wa fedha 2021/2022, jumla ya sampuli 215 za dawa zilifuatiliwa na kuchunguzwa ambapo matokeo ya uchunguzi yalionesha kuwa dawa zote sawa na 100% zilifaulu vipimo vya kimaabara.

Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi huyo wakati akieleza utekekezaji wa shughuli za mamlaka hiyo kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023  alisema vifaa tiba na vitendanishi, jumla ya sampuli za matoleo 567 zilichunguzwa na sampuli 522 sawa na 92% zilikidhi vigezo.

"Hiki ni kiashiria kuwa kiasi kikubwa cha bidhaa za dawa na vifaa tiba kilichoko kwenye soko la Tanzania kinakidhi vigezo vya ubora" Alisema Fimbo.

Alisema Idadi ya majaribio ya dawa yaliyoidhinishwa imefikia 34 kwa mwaka 2021/22. TMDA hutathmini na kuidhinisha majaribio ya dawa yanayofanyika kwa binadamu hapa nchini ili kuhakikisha yanazingatia sheria, kanuni, miongozo na vigezo vya kulinda afya ya wale wanaofanyiwa majaribio hayo.

Fimbo alisema katika mwaka 2021/22, jumla ya tani 35,547.47 za bidhaa za dawa na vifaa tiba visivyofaa kwa matumizi ya binadamu zenye thamani ya takribani TZS 35.53 bilioni zilizoteketezwa.

Aidha alisema jumla ya kiasi na thamani ya bidhaa za dawa na vifaa tiba visivyofaa kwa matumizi ya binadamu zilizoteketezwa imeongezeka kutoka tani 14,704.80 zenye thamani ya TZS 8.5 bilioni zilizoteketezwa mwaka 2020/21 na kufikia jumla ya tani 35,547.47 zenye thamani ya takribani TZS 35.53 bilioni zilizoteketezwa mwaka 2021/2022.

Alisema kuhusu udhibiti wa bidhaa za tumbaku Mamlaka iliandaa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano (2021-26) wa Kitaifa wa Kupambana na Tumbaku pamoja na Mpango Kazi wa Miaka Mitano wa Udhibiti wa Tumbaku ambao umeanza kutekelezwa.

"Mamlaka iliandaa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano (2021-26) wa Kitaifa wa Kupambana na Tumbaku pamoja na Mpango Kazi wa Miaka Mitano wa Udhibiti wa Tumbaku ambao umeanza kutekelezwa" Alisema

"Tumeweka tayari mfumo wa udhibiti wa bidhaa hizi na hadi sasa tumekwishatambua bidhaa zote za tumbaku zilizoko kwenye soko ambapo idadi yake hadi sasa ni bidhaa 51,"

Aliendelea kueleza kuwa " Mamlaka imeanzisha maabara ya upimaji wa bidhaa za tumbaku kwenye jengo lake lililoko hapa Dodoma," Alisema Mkurugenzi huyo.

Aidha alisema ufuatiliaji wa madhara yatokanayo na matumizi ya bidhaa Mamlaka imeweka mifumo madhubuti ya ufuatiliaji wa madhara yatokanayo na matumizi ya dawa, chanjo na vifaa tiba (kitaalam vigilance system) ili kuweza kubaini, kutathmini na kuzuia madhara yasiyovumilika yasitokee kwa wananchi.

 Aidha, alisema  ili kuimarisha upatikanaji wa taarifa hizo, TMDA imeanzisha mfumo wa kielektroniki ujulikanao kama ADR Reporting Tool wa utoaji wa taarifa za madhara yatokanayo na matumizi ya dawa kwa kutumia simu za mkononi au kompyuta na kwa njia ya kutuma ujumbe mfupi kwenye simu.

Kupitia mfumo huu TMDA imepokea jumla ya taarifa 4,898 katika kipindi husika na hadi sasa kuna jumla ya taarifa 31,666 kwenye mfumo wa taarifa unaosimamiwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) ujulikanao kama Vigibase.

No comments:

Post a Comment

Pages