Adeladius Makwega-CHAMWINO IKULU
Kuna wakati pahala fulani Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam walikuwa wakifanya uchaguzi wa jumuiya zake ndogo ndogo, nafasi zikatangazwa na kutoa fursa kwa waombaji kuomba. Katika jumuiya moja hakukujitokeza mtu kuomba nafasi, kanisa hilo liliwahamasisha wanajumuiya kuomba nafasi hizo.
Mwenyekiti wa parokia hiyo alifika katika jumuiya hii na kupita nyumba kwa nyumba kuwahamasisha. Kazi ya mwenyekiti wa parokia ikazaa matunda na ndugu wawili wa familia moja walijitokeza kugombea nafasi ya mwenyekiti wa jumuiya.
La kustajabisha ndugu hao walikuwa baba na mwana,
”aha kulikoni tena baba na mtoto wanagombea nafasi moja?”
Wanajumuiya hii waliona wamekombolewa na muitikio wa familia hii ya wacha Mungu. Japokuwa hilo liliwashangaza mno lakini kukombolewa kulikuwa muhimu kuliko kustajabu.
Mwanakwetu siku ya uchaguzi ilifika na baba na mwana kusimama mbele kuomba kura kwa wanajumuiya hiyo.
“Jamani hata mwanangu nayeye anashindana na mimi, hii inaonesha namna nilivyomlea kiroho vizuri, sasa ninawaombeni mtimize haki yenu kwa kunipigia kura mimi.” Baba huyu alianza kuomba kura na kumalizia kwa kueleza uzoefu wake wa uongozi wa kiroho na kijamiii.
Wanajumuiya hii walioshiriki uchaguzi huo walikuwa wengi mno siyo kawaida hata wale wanajumuiya goigoi walikuwepo na hilo lilihamasisha mno wakatoliki hao kushiriki pamoja uchaguzi huo. Wanajumiya hii walianguka vicheko vya bashasha kwa tukio walilokuwa hawajawahi kulishuhudia maishani mwao iwe kwenye dini au kwenye siasa.
Kristo … Tumaini letu, Tumsifu Yesu Kristo … Milele Amina…
“Jamani niliyesimama mbele yenu ni mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa jumuiya, nimeshawahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi katika dini na taasisi mbalimbali. Nina hakika mkinichagua kuwa mwenyekiti wa jumuiya hii nitawaongoza vizuri sana.”
Mgombea huyu kijana aliendelea kusema kuwa anatambua kuwa mgombea mwezake ameshaoamba kura na ni baba yake mzazi, yeye ndiye aliyemfundisha dini na kumpeleka kanisani, lakini huo ulikuwa wajibu wake kama mzazi kwa mwanawe.
“Hiki kisiwe kigezo cha yeye kupigiwa kura, naombeni mnichague niwe mwenyekiti wenu.”
Basi wanajumuiya hawakuwauliza maswali yoyote kwa kuwa walikuwa na sababu nyingi; mojawapo ni kuokoa kwao jahazi la jumuiya yao iwe na mwenyekiti. Kura zikapigwa vizuri sana na baba akamshinda mtoto wake kwa kura chache mno.
Binafsi baada ya tukio hilo nilifuatilia kulikoni?
Niligundua kuwa katika uongozi wa dini panapotokea mgogoro katika uongozi hilo linakuwa suala la kiimani na watu wengi wanaogopa sana kuharibu katika imani zao. La pili katika uongozi wa dini walio wengi hawawezi kufanya watakavyo kinyume na kwenye siasa ya kidunia huko watu wanafanya watakavyo.
Nilijaribu kulihusisha tukio hili na uongozi wa siasa kidunia mathalani mkitangaza nafasi alafu watu hawajitokezi, mnaongeza muda watu hawajitokezi, kazi inayofuta wale wa zamani wanaendelea kwa muda wakati mnafanya mchakato wa kuwashawishi wale mnaowaona wanasifa.
Mkiwashawishi wenye sifa alafu wakagombea hapo mtapata viongozi wazuri mno na wataungwa mkono na jamii. Hapo hata yule aliyeshawishika kuongoza ataongoza kwa kipindi kilichopangwa tu akimaliza anakuja mwingine na siyo kung’ang’ania nafasi hiyo.
Katika kisa hiki baba huyu aliyeshinda aliiongoza jumuiya vizuri sana kama miongozo ya jumuiya ilivyo kwa kuheshimu dini yake, kuheshimu waliomshawishi na kuheshimu waliompigia kura. Jumuiya hii waliishi vizuri wakishirikiana kwa kila jambo na tukio kama hilo halikutokea tena.
Mungu bahati baada ya miaka 20 mgombea yule kijana wa nafasi ya uenyekiti wa jumuiya hii aligombea ubunge wa Malinyi na kushinda na sasa ni mbunge wa Malinyi mkoani Morogoro, mheshiwa Antipas Zeno Mngungusi
Mwanakwetu upoo
Nakutakia siku njema.
0717649257
No comments:
Post a Comment