HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 31, 2022

Afya ni rasilimali muhimu

Ifahamike kwamba, jamii zote duniani hutegemea rasilimali afya ili kuzifanya jamii hizo kujiendeleza na
kupiga hatua za maendeleo. 

 

Afya ni rasilimali muhimu na ni haki inayopaswa kulindwa. Kukithiri kwa malalamiko na ukosoaji juu ya mwenendo wa upatikanaji na ugharamiaji wa huduma ya afya nchini
kwetu umetusukuma sisi ACT Wazalendo kuzungumza na wananchi.


Sisi wote ni mashahidi namna ndugu zetu, jamaa na marafiki wanavyopoteza maisha kwa kushindwa kumudu gharama za matibabu. Mara kadhaa, ndugu wa marehemu kuzuiwa kuchukua maiti katika hospitali kutokana na marehemu kuwa na deni linalotokana na gharama za matibabu. Utu katika taifa
letu unafifia kutokana na kukosa mfumo Madhubuti wa afya.


Kukosekana kwa mfumo rasmi wa hifadhi ya jamii kumewafanya watu wengi wasiwe na uwezo wa
kupata huduma za matibabu. 

 

Kwahiyo, leo tutaenda kuzungumzia mambo mawili; Mosi, suala la bima ya afya na mfumo mzima wa ugharamiaji wa huduma ya afya na pili, mfumo wa hifadhi ya jamii kama njia ya kujenga utaratibu madhubuti wa kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma bora ya afya.
 

1: Mfumo wa sasa wa Bima ya afya unatengeneza na kuimarisha matabaka nchini:


Mfumo uliyopo hivi sasa umefanya upatikanaji wa huduma za afya kwa sehemu kubwa kutegemea na uwezo wa pesa alionao mwananchi kununua huduma hiyo badala ya uzito wa ugonjwa wenyewe. 

 

Hii imetokana na sera ya mwaka 1990 iliyolenga kurekebisha uchumi na soko huria ambapo, Serikali ilianza kutekeleza sera ya uchangiaji wa huduma muhimu kama vile Afya na Elimu. Matokeo ya mfumo huu nchini umekuwa kuongezeka pengo kubwa la wananchi wenye nacho na wasio nacho katika
kupata huduma za afya.


Mfumo wa sasa wa ugharamiaji wa huduma za afya umeachwa kwenye mabega ya mwananchi aidha kwa kutumia pesa taslimu au kwa kupitia mfumo wa Bima ya Afya ambao bado haukidhi sehemu kubwa ya matibabu. 

 

Serikali haijaweka jitihada zozote katika kuhakikisha kila mtanzania anapata huduma za afya kwa usawa kwa kudhibiti gharama kubwa ya matibabu na mifumo mibovu inayoshindwa kuunganisha nguvu za wananchi na kupanua wigo na uwezo wa Serikali kugharamia huduma.


Takwimu za Hali ya Uchumi wa Taifa zilizotolewa mwezi Juni mwaka huu (2022), zilionyesha kwamba mwaka 2021 jumla ya Watanzania milioni 41 (41,448,117) walikuwa wagonjwa wa nje kwenye Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati zote nchi nzima. 

 

Hii ina maana kuwa 71.8% ya Watanzania waliumwa mwaka 2021. Katika nchi ambayo raia wake wanaumwa kwa kiwango hiki suala la Afya linatakiwa kuwa kipaumbele cha Serikali na kuchukuliwa kwa uzito mkubwa. Kitendo cha Serikali
kujiondoa kwenye kuhudumia raia wake kwenye afya kwa namna yoyote ni kuumiza wananchi.


A: BIMA ya Afya (NHIF) sasa ni biashara siyo huduma


Kila uchao Serikali inabuni mipango ya kugeuza NHIF kutoka kuwa Bima ya umma kwenda kuwa Bima Binafsi. Hii inatokana na mtazamo wa kibiashara katika uendeshaji wa Mfuko wa taifa wa bima ya afya (NHIF), mtazamo ambao una lenga kulimbikiza faida na kukwepa wajibu wa Serikali kuwahudumia wananchi wake. 

 

Ndio maana mara kadhaa, Serikali au watendaji wa mfuko wanajitokeza kujenga hoja za kupunguza huduma zinazotolewa na BIMA kwa kuweka madaraja, kupandisha gharama, kuondosha baadhi ya huduma na kuzuia matumizi kwa baadhi ya hospitali.

Aidha, kwa kutumia mtazamo huu Serikali inategemea gawio au kuchukua fedha za mfuko jambo linapelekea Mfuko wa NHIF kujiendesha kwa hasara. 

 

Mathalani, mwenendo wa Mfuko wa Bima ya Afya kujiendesha kwa hasara kwa miaka takribani mitatu mfululizo kuanzia 2018/19 hadi 2021/22 zinatokana na madeni yaliyokopwa na Serikali. 

 

Hivi karibuni, kila mara mfuko wa bima umekuwa ukileta vifurushi vipya ili kufidia makosa yake kwa kuwatoza wananchi gharama zaidi na kupunguza mafao wanayopata wananchi wanapoumwa. Wananchi hawakupaswa kutumika kulipia gharama za maamuzi mabovu ya Serikali.


Mfuko huu wa NHIF kwa sasa unaendelea kuendeshwa kwa hasara, na kwa mwaka 2020/21 mfuko umepata hasara ya shilingi bilioni 109.71. 

 

Katika ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa hesabu za Serikali 2020/21 udhaifu wa kiutendaji wa NHIF ambao ulisababisha hasara ya mabilioni ya fedha
yanayotokana na ukusanyaji hafifu wa madeni, utoaji mikopo na uwekezaji mbovu wa fedha za umma.


B: ACT Wazalendo inaamini, Hifadhi ya Jamii italeta BIMA ya afya kwa watanzania wote Sehemu kubwa ya watanzania wamejiajiri mashambani au wapo kwenye sekta isiyo rasmi ambayo inachukua asilimia 52 ya nguvu kazi yote nchini. 

 

Watu walio katika ajira rasmi (kwenye sekta ya umma na binafsi) ni watu milioni 3.5 sawa na asilimia 14.2 pekee. Watu wote wasiokuwa kwenye ajira rasmi hawana mfumo mzuri wa matibabu, pensheni, likizo au mapumziko ya uzazi wala kulindwa kutokana na majanga. 

 

Sisi, ACT Wazalendo tuna amini kuwa ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma ya matibabu kupitia huduma ya bima ya afya kwa wote tunapaswa kuunganisha mfumo wa hifadhi ya jamii kwa kila mtanzania ili anapochangia hifadhi ya jamii awe anapata huduma ya afya moja kwa moja. Watanzania waunganishwe na NSSF ili kupanua fao la matibabu kutoka idadi ya sasa ya asilimia moja.


Kwa mujibu wa taarifa za wizara ya Afya, jumla ya watanzania 8,224,271 sawa na asilimia 14.7 ya watanzania wote (takriban milioni 59.4) ndiyo wanaonufaika na huduma za bima ya afya.


Mfuko wa NHIF kwa sasa unahudumia wanachama 1,127,956 na wanufaika 4,341,993 sawa na asilimia 8 tu ya Watanzania wote, huku asilimia 5.4 wanahudumiwa na Bima ya afya ya jamii iliyoboreshwa (iCHF), asilimia 0.3 ya wanufaika wamejiunga kupita SHIB-NSSF na asilimia 1 wanatumia bima za makampuni binafsi. Kwa hiyo, 85.3% ya nguvu ya Watanzania haimo kwenye Mfumo wa Bima ya Afya, jambo ambalo halikubaliki.
 

ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kuhakikisha kila mtanzania anakuwa kwenye mfumo wa hifadhi ya jamii ili kuwawezesha wananchi wote kupata bima ya afya ya taifa.


Pili, ACT Wazalendo inaitaka Serikali kupitia wizara ya fedha ihakikishe mikopo inayodaiwa kupitia mashirika ya Umma na Wizara kurudishwa haraka ili kuupa uwezo Mfuko wa Bima wa Afya kujiendesha wenyewe.


Tatu, Serikali isimamie uwekezaji unaofanya mfuko wa taifa wa bima ya afya kuhakikisha unaleta tija
katika mapato yake.


Hitimisho;


ACT Wazalendo inaamini katika upatikanaji wa Bima ya Afya kwa Watanzania wote na hili tuliliweka
wazi katika ilani yetu ya mwaka 2020. Ni ahadi yetu kwa wananchi wote, tutaendelea kupigania
upatikanaji wa huduma bora ya afya kwa wananchi wote bila kujali kipato chao.

No comments:

Post a Comment

Pages