Serikali ya Tanzania na Singapore zimeahidi kuendelea kuimarisha
ushirikiano wa kidiplomasia na kihistoria uliopo baina yao ili kutekeleza kwa
ufanisi malengo ya kiuchumi ya mataifa hayo.
Ahadi hiyo imetolewa wakati wa mazungumzo kati ya Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula na
Balozi wa Singapore nchini mwenye makazi yake Singapore, Mhe. Douglas Foo yaliyofanyika
tarehe 30 Agosti 2022 katika ofisi za Wizara jijini Dodoma.
Katika mazungumzo hayo Mhe. Balozi Mulamula alieleza kuwa ni
muhimu kwa Tanzania na Singapore kuuenzi ushirikiano ulioasisiwa na waasisi wa
mataifa yao kwa manufaa ya wananchi wake.
Pia alieleza Tanzania ina nia ya kushirikiana na Singapore
katika maeneo mbalimbali ikiwemo: Kukuza shughuli za bandari, kilimo cha
mbogamboga na matunda, usafirishaji wa mazao ya biashara kama vile kahawa na
chai, biashara, utalii, ufadhili wa masomo na ushirikiano katika masuala ya utamaduni
hususan kuanzisha makubaliano ya kufundisha lugha ya Kiswahili nchini
Singapore.
Maeneo mengine ya ushirikiano ni pamoja na: Kujenga uwezo
katika masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano, uwekezaji katika maeneo
maalum ya viwanda, usafiri wa anga na ushirikiano katika masuala ya kikanda.
“Tanzania inawekeza katika kujenga uwezo wa rasilimali watu kwenye
masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano, pia kupitia uwepo wa mkongo wa
mawasiliano wa taifa ina dhamira ya kutoa huduma ya mawasiliano nje ya mipaka
yake” alisema Balozi Mulamula.
Kwa upande wa Mhe. Douglas Foo alieleza kuwa uhusiano kati ya
Tanzania na Singapore unatimiza miaka 40 tangu ulipoanzishwa hivyo, ni muhimu
kuangalia maeneo yenye fursa za kiuchumi ili kuendelea kuimarisha ushirikiano
kwa manufaa kwa pande zote mbili.
Tanzania na Singapore zinaunganishwa na uanachama wao katika
Umoja wa nchi za jumuiya ya madola na hivyo ni fursa kwa mataifa hayo kuongeza
maeneo ya ushirikiano kupitia makubaliano yatakayowezesha usimamizi wa karibu wa
utekelezaji wa malengo katika maeneo husika ya maendeleo.
Mhe. Douglas Foo akifafanua juu ya uzoefu wa Singapore katika kusimamia makubaliano mbalimbali yanayoanzishwa na serikali yake kwa lengo la kukuza uchumi na kuinua maendeleo ya Taifa kwa ujumla. |
Mazungumzo yakiendelea. |
Mhe. Balozi Mulamula akiagana na Mhe. Foo baada ya mazungumzo. |
No comments:
Post a Comment