September 09, 2022

NSSF yakusanya Sh Trilioni 1.42, yataja vipaumbele vyake mwaka wa fedha 2022/23

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam kuhusu taarifa ya utendaji na vipaumbele vya mfuko huo kwa mwaka wa fedha wa 2022-23.
 

 

Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam


Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umesema kuwa katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2022 umekusanya  Sh trilioni 1.42 ukilinganisha na Sh trilioni 1.38 waliyopanga kukusanya.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba wakati akitoa taarifa ya utendaji na vipaumbele vya mfuko huo kwa mwaka wa fedha wa 2022/23.

Amebainisha kuwa wamekusanya kiasi hicho cha fedha kutokana na uboreshaji wa huduma zao ikiwemo matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kwamba mwanachama anaweza kupata huduma bila kufika ofisi za NSSF kwa kutumia mifumo ya waajiri na wanachama.

" Ili tuweze kulipa mafao ya wanachama lazima tuwekeze michango yao kwenye miradi salama tukifanikiwa kwenye hilo mfuko utaendelea mafao ya wateja bila kupokea malalamiko," amesema Mshomba.

Amesisitiza kuwa katika mwaka wa fedha 2022/23 mfuko huo umepanga kutekeleza vipaumbele mbalimbali ikiwemo kuongeza idadi ya wanachama kuifanya NSSF iendelee kukua na kua endelevu, kuimarisha mifumo na udhibiti wa ukusanyaji michango kwa kutumia TEHAMA pamoja na kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wao.

Ameongeza kuwa watawekeza kwenye miradi salama ili kuepusha upotevu wa fedha za mfuko pamoja na kukamilisha miradi iliyokwishaaza ikiwemo Mradi wa Jengo la Biashara Mwanza, Jengo la Mzizima na Miradi ya Nyumba za Makazi zilizopo Kigamboni na Tuangoma.

Amefafanua kuwa vipaumbele vingine ni kutekeleza mkakati wa mpango wa uchangiaji kwa hiari hasahasa kuongeza wanachama wasio kwenye sekta rasmi na utoaji elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa mfuko wa jamii.

Pia amesema watapitia mpango wa maendeleo ya muda mrefu utakaoishia mwaka wa fedha huo na kutilia mkazo miradi ya mfuko huo iliyokwishaanza ina thamani yake ni Sh Bilioni 691.

Katika hatua nyingine, amesema thamani ya mfuko imekuwa kwa kasi ukilinganisha na miwili iliyopita ilikuwa Sh Bil 4.3 ambapo hivi sasa imefikia Sh trilioni 6.2.

Amewahamasisha Watanzania kushiriki kwenye Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Agosti 23 mwaka huu kwa ajili mipango ya mendeleo ya nchi.


No comments:

Post a Comment

Pages