October 06, 2022

NMB yaihakikishia JWTZ udhamini zaidi CDF Trophy

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania , Jenerali Jacob Mkunda akimkabidhi Kikombe mshindi kutoka timu ya NMB, Bw. Abdallah Gunda kwenye mashindano ya NMB CDF TROPHY 2022, yaliyofanyika katika viwanja vya Golf Lugalo, Dar es Salaam. Kulia ni Afisa Mkuu wa Biashara na wateja Binafsi, Bw. Filbert Mponzi na kushoto ni Mkuu wa Majeshi wa Malawi, Generali Vincent Nundwe.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Jacob Mkunda akimkabidhi Kikombe mshindi kutoka timu ya NMB, Bw. Sigfrid Ophishas kwenye mashindano ya NMB CDF TROPHY 2022, yaliyofanyika katika viwanja vya Golf Lugalo, Dar es Salaam. Kulia ni Afisa Mkuu wa Biashara na Wateja Binafsi, Filbert Mponzi na kushoto ni Mkuu wa Majeshi wa Malawi, Generali Vincent Nundwe.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Jacob Mkunda akimkabidhi Kikombe na zawadi mshindi wa Jumla wa mashindano ya NMB CDF TROPHY 2022, Cpl ,Malius Kajuna, yaliyofanyika katika viwanja vya Golf Lugalo, Dar es Salaam. Kulia ni Afisa Mkuu wa Biashara na Wateja Binafsi, Bw. Filbert Mponzi na kushoto ni Mkuu wa Majeshi wa Malawi, Generali Vincent Nundwe.

Picha ya pamoja.


NA MWANDISHI WETU

 

BENKI ya NMB imemhakikishia Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania (CDF), Jenerali Jacob Nkunda, udhamini endelevu wa Mashindano ya Gofu ya Mkuu wa Majeshi (NMB CDF Trophy), ambayo ni sehemu ya maadhimisho ya kuzaliwa kwa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

 

Ahadi hiyo imetolewa na Afisa Mkuu wa Biashara na Wateja Binafsi wa NMB, Filbert Mponzi, wakati wa hafla ya utoaji zawadi kwa washindi wa NMB CDF Trophy 2022, iliyofanyika katikaVviwanja vya Gofu Lugalo jijini Dar es Salaam, ambako kwa siku mbili wakali wa mchezo huo wapatao 243 walichuana.

 

Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Mkuu wa Majeshi Mstaafu Tanzania Jenerali George Waitara na Mwenyekiti wa Klabu ya Gofu Lugalo, Brigedia Jenerali Michael Luwongo (Mstaafu), pamoja na Mkuu wa Majeshi wa Malawi, Jenerali Vicent Nundwe, aliyeambatana na nyota wa timu za Jeshi la Malawi.

 

Awali akiwasilisha salamu za Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna na Mwenyekiti wa Bodi, Dk. Edwin Mhede, Mponzi alimpongeza Jenerali Nkunda kwa kuaminiwa na Rais Samia Suluhu Hassan na kuteuliwa, na kuahidi kumuunga mkono ili kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

 

“Kwa kutambua umuhimu wa mchezo wa gofu, lakini pia mahusiano ya NMB na JWTZ, tumeona umuhimu wa kuendelea kudhamini mashindano haya ya Mkuu wa Majeshi na tumefanya hivyo kwa miaka sita sasa. Mwaka huu katika CDF Trophy, NMB imetoa shilingi milioni. 60 za kugharamia zawadi na vifaa mbalimbali. 

 

“Nikuahidi CDF Nkunda, NMB tukiwa benki ya kizalendo, benki ambayo Serikali ina hisa za kutosha na ukweli kuwa sisi ni wadau wakubwa wa Serikali na kwa kutambua umuhimu wa JWTZ, tutaendelea kudhamini CDF Trophy kwa miaka mingi ijayo.

 

Aliongeza “Kwa hiyo, mnapaswa kutambua kwamba mtakuwa na sisi kwa miaka mingi ijayo katika mashindano haya, ambayo tumeyasapoti majeshi yetu katika mashindano mengi inayoshirikisha timu za majeshi yetu kitaifa na kimataifa,” alisisitiza Mponzi.

 

Aidha, Mponzi pia aliahidi kugharamia ununuaji wa viatu na jezi kwa ajili ya watoto walioshiriki mashindano hayo, baada ya kupokea ombi kutoka kwa kocha wa vijana hao.

 

“Jioni wakati tunakabidhi zawadi za watoto (juniors),kocha alilalamika vijana wake kukosa viatu, nasi NMB tukalichukua hilo, baada ya kuambiwa Sh. Milioni 5 zinatosha kuwezesha vijana wale kupata viatu na jezi ili kuwachagiza kushiriki kwa ufanisi mchezo huu na kupata mafanikio,” alisema.

 

Mponzi alitumia nafasi hiyo kumueleza Generali Nkunda kuwa NMB inayo Matawi Maalum kadhaa nchini kwa ajili ya maofisa ‘private banking’ na kwamba kwa Dar es Salaam, wana matawi ya Oyster Plaza na Makao Makuu, hivyo kuwakaribisha majenerali wa jeshi na maofisa wengine kufika kuhudumiwa.

 

Kwa upande wake, Jenerali Nkunda alianza kwa kuipongeza na kuishukuru NMB kwa kudhamini uliofanikisha mashindano hayo kwa kiwango cha kimataifa,  huku akisisitiza kuwa matumaini yake ni benki hiyo kuendelea kuisapoti JWTZ na kuiunga mkono Serikali.

 

“Nimefurahishwa na udhamini wa NMB kwa mwaka wa sita mfululizo sasa, hii inaonesha na kuthibitisha ni kwa namna gani NMB ilivyo karibu na JWTZ, lakini pia inatumia fursa hiyo kurudisha fadhila kwa jamii.

 

“Nitoe wito kwa taasisi za Serikali na mashirika mengine kuiga mfano wa NMB na wadhamini wengine katika kushirikiana na jeshi kwa kudhamini mashindano haya na pia kusaidia ushiriki wa timu za majeshi katika Mashindano ya Majeshi ndani nan je ya nchi,” alisisitiza. 

 

Generali Nkunda aliongeza kuwa NMB CDF Trophy ni shindano lenye historia ndefu na umuhimu wa kipekee katika historia ya JWTZ, na kufichua kuwa baada ya uteuzi wake, alikabidhiwa ulezi wa timu na mtangulizi wake Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Venance Mabeyo, huku akiahidi kuyaboresha ili kuyaongezea mvuto.

 

“CDF Trophy ni shindano la kuadhimisha kuzaliwa kwa JWTZ, ambayo huwa ni Septemba 1 kila mwaka, lakini mwaka huu kutokana na sababu mbalimbali likasogezwa mbele. Tunamshukuru Mwanzilishi Jenerali Waitara na walioliendeleza, kwani JWTZ ni kisima cha kuendeleza michezo,” alibainisha.

 

Jenerali Nkunda alimpongeza CDF wa Malawi, Vicent Nundwe kwa kuacha majukumu yake na kuja kushiriki CDF Trophy 2022 yeye na timu za maofisa wa Jeshi la Malawi, ushiriki ambao umeliongezea shindano hilo hadhi kimataifa.

 

Katika mashindano hayo yaliyoanza Oktoba 1, Koplo Marius Kajuna aliibuka mshindi wa jumla wa CDF Trophy, yaliyohusisha kategori za ‘Combat Competition,’ ‘Professional,’ ‘Main Event CDF Trophy,’ ‘Juniors’ na ‘Sponsors Competition,’ ambako Abdallah Gunda wa NMB aliwagaragaza wadhamini wengine.

No comments:

Post a Comment

Pages