Na Tullo Chambo
ALIYEWAHI
kuwa Katibu wa Kamisheni ya Wachezaji Shirikisho la Riadha Tanzania
(RT), Tabu John Jilala Mwandu, amejitosa rasmi kugombea nafasi ya ujumbe
Kanda ya Pwani katika uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika jijini
Dodoma, Novemba 27 mwaka huu.
Mwandu, alirejesha rasmi fomu ya kugombea katika ofisi za RT jijini Dar es Salaam leo Novemba 15 majira ya saa 7: 15 mchana.
Akizungumza
mara baada ya kurejesha fomu, Jilala, alisema ametekeleza takwa la
kikatiba, na kwamba wadau wa mchezo wa riadha wawe watulivu kipindi hiki
kwani mambo mazuri yanakuja.
"Nimetekeleza kwanza
takwa la kikatiba kuchukua na kurejesha fomu, wadau wa riadha wawe na
subira hadi pale kipyenga rasmi cha kampeni kitakapolia nitaanika sera
zangu na wajumbe watapima, Ila mambo mazuri yanakuja," alisema Jilala.
Jilala
anakuwa mgombea wa kwanza kurejesha fomu kugombea kuwakilisha Kanda ya
Pwani, inayojumuisha mikoa ya Pwani, Dar es Salaam, Lindi na Mtwara.
Zoezi la kurejesha fomu kwa wagombea, linatarajiwa kufikia tamati Novemba 20 mwaka huu.
Wengine waliokwisha rejesha fomu ni Kanali mstaafu Juma Ikangaa, Mohammed Kiganja na Suleiman Nyambui.
RT
inatarajiwa kufanya uchaguzi huo, kuziba nafasi za Makamu wa Rais na
Mjumbe Kamati ya Utendaji Kanda ya Pwani, ambazo ziko wazi baada ya
waliokuwa wakizishikilia kujiuzulu kutokana na sababu mbalimbali.


No comments:
Post a Comment