Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Peof. Adolf Mkenda, akimkabidhi cheti mmoja wa wanafunzi waliofanya vizuri wakati wa mahafali ya kidato cha nne ya shule za sekondari za kiislam mkoani Dar es Salaam.
NA ASHA BANI
SERIKALI imesema haitamfumbia macho mwalimu anayevunja maadili kwa kufanya mapenzi na mwanafunzi na kwamba hatua kali za kisheria dhidi yao itachukuliwa.
Hayo yalielezwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Peofesa Adolf Mkenda wakati wa mahafali ya kidato cha nne ya shule 11 za kiislamu Jijini Dar es Salaam.
Amesema tabia hizo zinazofanywa na baadhi ya walimu kuwa na mahusiano na wanafunzi, kwa kusema hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Amesema atakutana na waendesha mashtaka wanaosimamia kesi hizo ili kusimamia kesi hizo kwa haraka na hatua kali dhidi yao zichukuliwe.
Anasema wanalazimika kuwa wakali zaidi na kwamba anatoa tahadhari kwa walimu na wenye shule kusimamia malezi kwa vijana,.
" Nalaani vikali sana wale walioruhusu mchezo huo Kisarawe. Hairuhusiwi na tunalaani zaidi vitendo vile tutachukua hatua zaidi," alisema.
Alisema walimu na wamiliki wa shule wana majukumu hivyo kinachotakiwa ni watoto kupata malezi ambayo wazazi wanatarajia.
Katika hatua nyingine alishukuru shule binafsi kwa kueleza kuwa wanapotoa elimu bora wanaongeza ubora wa elimu, hali iliyosababisha wazazi kuacha kupeleka watoto kusoma nchini Kenya na Uganda.
Lakini pia alisema lipo suala la mitaala pamoja na masomo ya dini, hivyo kama alivyoombwa atashughulikia suala la combination ili kiarabu kiwepo.
Awali Sheikh Mkuu wa Dar es Salaam, ambaye ni mlezi wa shule za kiislam Dar es Salaam, Alhad Mussa aliwausia wanafunzi waliomaliza waendelee kushikamana na maadili.
" Elimu bila maadili haina maana mbele ya taifa linalowategemea kama viongozi wa kesho," alisema.
Alisema taifa likikosa maadili ni sawa na kusema hilo ni taifa mfu.
Wanafunzi waliohitimu waliotoka sekondari za Ilala Islamic, Qiblatain, Dar es Salaam Islamic, Kunduchi Girls Islamic, Al-haramain, Ununio Boys Islamic, Muzdalifa na Temeke Islamic.





No comments:
Post a Comment