HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 08, 2023

 KAMATI YA UTATUZI WA MIGOGORO VIJIJI NA MITAA 975 NCHINI YAHITIMISHA KAZI DAR ES SALAAM


Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendelo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula akiongea na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani kuhusu zoezi la utatuzi wa migogoro ya ardhi ya Mitaa na Vijiji 975 zoezi ambalo limehitimishwa leo Mkoani Dar es Salaam.

 

Na Anthony Ishengoma

 

Kamati ya Mawaziri nane ya kutatua migogoro ya ardhi kati ya Vijiji na Mitaa 975 imehitimisha kazi yake katika Mkoa wa Dar es Salaam baada ya kamati hiyo na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani kukutana jana Mkoani Dar es Salaam na kukubaliana kuwa wananchi wa kata ya Zingiziwa sasa ni wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam. 

 

Awali akiongea na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alisema kuwa kumekuwepo na migogoro ya mipaka kati ya baadhi ya maeneo ya Dar es Salaam na Pwani jambo ambalo limekuwa likizua taharuki kwa wananchi wa maeneo hayo ikiwemo suala zima la huduma za msingi ambazo zimekuwa zikitolewa katika mikoa yote miwili.

 

Waziri Mabula akiongea na vyombo vya habari mara baada ya kuhitimisha mkutano huo alibainisha kuwa baada ya zoezi hilo kuhitimishwa Mkoani Dar es Salaam maeneo mengine ambayo Rais wa Tanzania ameridhia yachukuliwe au yagaiwe kwa wananchi zoezi la kuyatambua na kuyawekea mipaka linaendelea katika maeneo hayo.

 

Aidha Dkt. Angeline Mabula aliongeza kuwa zoezi la utambuzi wa maeneo hayo litajulikana mpaka ifikapo mwezi Machi mwaka huu na kwa yale maeneo ambayo yatakuwa bado yana mkanganyiko wa mipaka Waziri mwenye dhamana atayapitia na kuyatolea majibu baada ya masuala ya kiutaalam kuwa yamefanyiwa kazi.

 

Waziri Mabula aliongeza kuwa kamati yake imebaini kuwa kuna sababu tatu zilizochangia Migogoro ya ardhi hiyo kuwepo mojawapo likiwa la wananchi kutotii sheria kuvamia maeneo ambayo hayaruhusiwi kuingia akiyataja maeneo ya ifadhi pamoja na maeneo ambayo yanamilikiwa na Taasisi mbalimbali ambazo zimeshindwa kulinda maeneo yake na hatimaye kuvamiwa wananchi na kujimilikisha kama vile ni mali yao.

 

Mbali na uvamizi wa ardhi Waziri Mabula alibainisha kuwa kuna baadhi ya maeneo baadhi ya wananchi wamekuwa wakitumia ardhi kinyume na sheria za kutunza mazingira ikiwemo kutofanya kilimo ndani ya mita sitini ya vyanzo vya maji hivyo watu kuendeleza kilimo katika kingo za mito na maziwa akibainisha kuwa wananchi wanafahamu kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha taratibu zilizopo.

 

Waziri Mabula aliongeza kuwa kamati yake imekuwa ikitoa elimu kwa wananchi kuhusu utunzaji wa vyanzo maji nakuongeza kuwa kila Waziri mwenye dhamana alikuwa akiongea na wananchi kuhusiana na eneo lake na Rais ameridhia maeneo ya ifadhi ambazo zimekosa sifa kugaiwa kwa wananchi kwa utaratibu maalum uliotolewa na serikali.

 

Waziri wa TAMISEMI Bi. Angela Kairuki alihitimisha majadiliano kati ya Mkoa wa Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani kwa kutumia mamlaka aliyonayo kama Waziri mwenye dhamana kwa kuamua wananchi wa Zingiziwa kubakia Mkoa wa Dar es Salaam na kuwataka viongozi wa Dar es Salaam kujipanga ili kuwatangazia wananchi wa Zingiziwa kwamba ni wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam.

 

Waziri huyo wa TAMISEMI aliwaagiza wakuu wa Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani Kwenda mapema kwa wananchi wa Zingiziwa ili kuwatangazia tamko la serikali wakati taratibu nyingine zikifuata zikiwemo taratibu za kitafsiri tamko la kiserikali kuhusu mipaka ili kuondoa mgogoro uliopo kiutawala.

 

Waziri Kairuki alibainisha kuwa maamuzi yake yamezingatia busara ikiwemo huduma za elimu, na masuala mengine kama vile huduma za sensa, usalama, utaratibu wa uandikishaji anwani za makazi lakini pia  uzoefu wa maeneo ambaya awali yalikuwa na migogoro kama hii ya kiutawala. 

 

Wizara vya Ardhi kwa kushiruikiana na Wizara za kisekta kwa muda sasa wamekuwa katika zoezi la utatuzi wa Migogoro ya Ardhi hususani kwa wananchi ambao wamekiuka taratibu za matumizi ya ardhi au kumiliki ardhi bila kuzingatia sheria na sasa kamati hiyo imehitimisha zoezi hili katika Mkoani Dar es Salaam.  

No comments:

Post a Comment

Pages