Baadhi ya wanariadha wa kike wanaotarajiwa kushiriki mashindano hayo.
NA TULLO CHAMBO, DAR ES SALAAM
CHAMA cha Riadha Zanzibar (ZAAA), kimesema kimejiandaa kuonyesha ushindani mkali kwenye mashindano ya Radha ya Wanawake maarufu kama 'Ladies First' yanayotarajiwa kufanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, Januari 21 na 22, 2023.
Akizungumza makao makuu ya Shirikisho la Riadha Tanzania (AT), jijini Dar es Salaam leo Januari 5, Kaimu Katibu Mkuu wa ZAAA, Muhidin Masunzu, alisema mara baada ya kupata rasmi barua ya mwaliko kutoka kwa waandaaji, mikoa yote mitano ya Zanzibar imejipanga vizuri kuelekea mashindano hayo.
Masunzu, alisema kila mkoa utawakilishwa na wanariadha sita, mmoja kati yao atakuwa ni wa Kurusha Mkuki, kama ambavyo waandaaji wameelekeza.
"Sisi Zanzibar huwa hatuna mashindano madogo, mikoa yote ya Zanzibar itashiriki kikamilifu na Insha Allah tuna uhakika nafasi zote tatu za juu tutazichukua," alisema Masunzu na kuongeza.
Na nichukue fursa hii kuwaomba na wenzetu wa Bara, wajipange hususan katika Kurusha Mkuki wasikose ili tuuinue mchezo huu, kama ambavyo waandaaji wamesisitiza.
Mashindano ya Ladies First hufadhiliwa na Serikali ya Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo la Kimataifa (JICA), chini ya uratibu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), na AT.
Wazo la kuanzishwa mashindano hayo, yenye lengo la kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika mchezo wa Riadha, liliasisiwa na Nguli wa Riadha, Kanali Mstaafu Juma Ikangaa.
ambaye pia ni Balozi wa Hiari JICA.
No comments:
Post a Comment