HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 14, 2023

TIMU YA TAIFA MBIO ZA NYIKA YATAKIWA KUIHESHIMISHA TANZANIA AUSTRALIA

Katibu Mtendaji BMT, Neema Msitha (kulia), akimkabidhi bendera ya Taifa, Nahodha wa Timu ya Taifa ya Mbio za Nyika, Fabian Sulle.


 


NA TULLO CHAMBO, RT

TIMU ya Taifa ya Mbio za Nyika inayotarajiwa kushiriki mashindano ya Dunia huko Australia Februari 18, imeagwa leo Februari 14 jijini Dar es Salaam, huku ikitakiwa kwenda kuipeperusha vema bendera ya Tanzania.


Wosia huo, umetolewa na Mgeni rasmi, Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha, wakati akikabidhi bendera ya Taifa, katika hafla iliyofanyika ukumbi wa Uwanja wa Taifa.


Msitha, mbali na kulipongeza Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), kwa kuiandaa timu hiyo, aliwataka wanariadha kutambua jukumu kubwa walilopewa la kwenda  kuwawakilisha Watanzania, hivyo wakajitume.


Msitha, alisema mashindano hayo ni fursa kwa wachezaji hao, kwani wakifanya vema watajitangaza zaidi kimataifa na kujiongezea kipato, kwani michezo hivi sasa ni ajira inayolipa sana.


"Tuna uhakika mmejiandaa vizuri, kwani baraza lilifuatilia kambi yenu Arusha, hivyo tunaamini mtakwenda kushindana na kutuletea ushindi, maana Watanzania wanafuatilia, hivyo muwaletee matokeo mazuri," alisema Msitha.


Awali, Rais wa RT, Silas Isangi, alisema timu imeandaliwa vizuri na anaamini wachezaji hao wanaokwenda wana uzoefu na kuwataka kwenda kujituma na kurejea na medali.
Naye Nahodha wa timu hiyo, Fabian Sulle, kwa niaba ya wachezaji, alisema wamejiandaa kimazoezi na wanategemea kurejea na ushindi.


Kocha wa timu hiyo, Denis Malle, alisema wamewaandaa vema wachezaji na wanawaahidi Watanzania matokeo mazuri.
 

Msafara wa timu hiyo yenye wachezaji wanne, ulitarajiwa kuondoka leo February 14 saa 9:45 kwa ndege ya Shirika la Oman, chini ya Mkuu wa Msafara, Wakili Jackson Ndaweka, ambaye ni Kaimu Katibu Mkuu RT.


           WACHEZAJI
1. FABIAN NELSON SULLE
Ndiye Nahodha wa timu, anatokea Timu ya Jeshi la Polisi.
Amezaliwa tarehe 1/10/1994 Guwang Mbulu mkoani Manyara.
Muda wake bora, Km. 21 ni 60:57, Km. 10 ni 28:01 na hii ni mara yake ya pili kushiriki Mashindano ya Nyika ya Dunia, mara ya kwanza ikiwa ni mwaka 2015 nchini China.

2. JOSEPHAT JOSHUA GISEMO
Naye anatokea Jeshi la Polisi Tanzania.
Amezaliwa tarehe 12/4/1992 Dareda Babati mkoani Manyara.
Muda wake bora, Mita 5000 ni 13:56, Mita 10000 ni 28:29 na Km. 21 ni 62:30 na hii itakuwa mara ya pili kushiriki Mashindano ya Nyika ya Dunia, mara ya kwanza ikiwa ni 2017 Kampala nchini Uganda.

3. INYASI NICODEMUS SULLEY
 Anatokea Klabu ya Talent ya jijini Arusha.
Amezaliwa tarehe 17/10/1998 Qorong'aida Karatu mkoani Arusha.


Muda wake bora, Km. 10 ni 28:32, Km. 21 62:22 na hii itakuwa mara yake ya kwanza kushiriki Mashindano ya Nyika ya Dunia.

4. MATHAYO SOMBI SAMHENDA
 Naye anatokea Klabu ya Talent jijini Arusha.
 Amezaliwa tarehe 26/2/1994 Balang'dalalu, Katesh Hanang mkoani Manyara.


Muda wake bora Km. ni 28:40, Km. 21 ni 63:10 na hii ni mara yake ya kwanza kushiriki Mashindano ya Nyika ya Dunia.

COACH
Denis Malle akitokea African Ambassador Athletics Club (AAAC), ya jijini Arusha.

No comments:

Post a Comment

Pages