HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 01, 2023

WAZIRI MASAUNI AFANYA ZIARA YA KUSHTUKIZA KITUO KIKUU CHA POLISI DODOMA, AHOJI MAHABUSU NA NDUGU ZAO WALIOFIKA KITUONI, WANANCHI WAPONGEZA ASKARI

 

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (kulia) akimsikiliza Mwananchi Judith Kizito wakati alipokuwa anazungumza na wananchi waliofika katika Kituo Kikuu cha Polisi Dodoma, alipofanya ziara ya kushtukiza kituoni hapo ya kukagua utendaji kazi, leo Februari 1, 2023. Wapili kulia ni Mkuu wa Kituo hicho, Namala Samson. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

 

Na Felix Mwagara, MoHA

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amefanya ziara ya kushtukiza Kituo Kikuu cha Polisi Dodoma kwa ajili ya kufuatilia utendaji kazi wa Kituo hicho.

 

Waziri Masauni aliwasili kituoni hapo Saa 6:02 mchana leo Februari 1, 2023 ambapo alikutana na wananchi mapokezi ya kituo hicho ambao walifika kwa ajili ya kuwachukulia dhamana ndugu zao waliopo katika mahabusu ya kituo hicho, aliwahoji kama wanapata huduma nzuri kutoka kwa askari wa kituo hicho.

 

Pia Waziri Masauni akiwa katika mapokezi ya kituo hicho, alikichukua kitabu cha taarifa za watuhumiwa wote waliopo mahabusu na baadaye kuelekea katika mahabusu hiyo na kuwaita baadhi ya watuhumiwa/mahabusu kituoni hapo na akiwahoji kwa kuwaita kwa majina kujua makosa yao yaliyoyafanya wawepo kituoni hapo.

 

Kabla ya kuzungumza na mahabusu hao, Masauni aliwataka wananchi wote waliofika kituoni hapo wakusanyike na kusikiliza kama wanamalalamiko yoyote la kutohudumiwa vizuri au changamoto zozote wanayotaka Waziri huyo azijue.

 

Mkuu wa Kituo cha Polisi hicho, OCS Namala Samson aliongoza kuwakusanya wananchi hao ambapo Waziri aliwataka waseme kama wanachangamoto yoyote ya kupata huduma kituoni hapo walizokutana nazo.

 

Mkazi wa Nzuguni, Isaya Mwaiga alisema Polisi Dodoma wanafanya kazi nzuri sana licha ya changamoto wanazokabiliana nazo, ikiwemo karatasi moja wanaandikia watuhumiwa wawili watatu, wanaukosefu wa karatasi wasaidiwe ili waweze kufanya kazi vizuri.

 

“Polisi Dodoma wanafanya kazi nzuri sana, Jana nimekuja kumtolea dhamana rafiki yangu, kwa muda niliokaa hapa nimejifunza kitu, kwanza vitendea kazi vya Polisi, hususani karatasi moja wanaandikia watu wawili watatu, wanahangaika sana, kama Waziri mwenye dhamana tunakuomba uwatazame Jeshi la Polisi kuanzia hapa Dodoma mpaka nchi nzima, tupo katika kutekelezani ilani ya Chama Cha Mapinduzi, laknii hawa pia wanasimamia ilani ya mama iweze kusimamiwa vema, wakitengenezewa mazingira mazuri ya kutoa huduma nzuri hata sisi mambo yetu yataenda vizuri” alisema Mwaiga.

 

Mkazi wa Kizota, jijini Dodoma, William Rashid alisema alifika kituoni hapo kumchukulia dhamana mke wake ambaye walifikisha kutokakna masuala ya vikoba lakini huduma ya dhamana imeenda vizuri na analipongeza Jeshi la polisi, lakini pia ameiomba Serikali kukiboresha kituo hicho kinakabiliwa na eneo dogo na wananchi wanaongezeka hivyo liboreshwe eneo hili ili waweze kupata huduma zaidi wakiwa wamekaa katika mazingira mazuri. 

 

Kwa upande wake, Ernest Mudanga, Mkazi wa Iyumbu jijini Dodoma, alifika kituoni hapo kufuatilia watu waliotapeli, amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kutoa huduma nzuri, alifika kituoni hapo jana, lakini walimpokea vizuri na anachosubiri kituo hapo ni mwenzake ili kufanikisha huduma yake ikamilike.

 

“Jeshi la Polisi linafanya kazi vizuri licha ya changamoto ndogondogo, nilifika jana kufuatilia watu waliotapeli, kwa kweli nimepewa huduma nzuri,” alisema Mudanga.  

 

Mkazi wa Michese, jijini Dodoma, Sostenes Mazengo amesema alifika kituoni hapo kumuombea dhamana ndugu yake lakini mlalamikaji hajafika, hivyo amemuomba Waziri huyo kusaidia endapo mlalamika anashindwa kufika watu waweze kusaidiwa kuliko kukaa muda mrefu kituoni.

 

Akizungumza na wananchi hao baada ya kuwasikiliza, Waziri Masaunia alisema alikuwa anapita katika kituo hicho akaamua kupita kituoni hapo kusikiliza wananchi na kukagua utendaji kazi wa Polisi.

 

“Nilikua napita hapa, nikaamua kuja kusikiliza wananchi na pia kukagua utendaji kazi, mmetoa maoni yaenu mimi nimefarijikia sana, hata wananchi miliopo hapa mnaridhika chombo ninachokisimamia mnaridhika na jinsi wanavyotekeleza majukumu yao, nataka niwahakikishie kutokana na changamoto za askari, Rais Samia toka aingie madarakani amefanya mambo mengi sana kuboresha jeshi la polisi,” alisema Masauni na kuongeza;

 

“Hata jana ameunda Tume kama mnafuatilia vyombo vya habari, pamoja na mambo mengine itaangalia maslahi ya askari matumizi ya mifumo ya kisasa, wakati mwingine unaweza ukalaumu askari kwasababu hawana nyenzo, anaweza akapita mhalifu lakini wakiwa na mifumo mizuri ya kuhudumia kwa haraka pengine wangeweza kufanikisha majukumu yao, kwa kipindi cha muda mfupi mtaona mabadiliko makubwa katika Jeshi letu la Polisi.”

 

Masauni aliongeza kuwa Rais Samia ameongeza ajira katika majeshi, ameboresha vitendea kazi na pia Jeshi lipo katika hatua ya mwisho ya ununuzi wa magari ya askari kwa wilaya zote Tanzania nzima na ametoa fedha karibu bilioni 15 kwa ajili ya kununua magari hayo. 

 

Pia alisema ujenzi wa vituo vya polisi umeshaanza, na pia kujenga nyumza za makazi unaendelea pamoja na kujenga vituo vya polisi nchini, pia amewapandisha vyeo askari na tangu aingie madarakani amewavisha vyeo askari wengi ambao ni zaidi ya 34,000 na mwaka huu 2023 watapandishwa wengine.

 

“Nimepita katika kituo hiki kama njia tu nilikua na shughuli hapo nikasema nisimame nikaaingia ndani, hamjapangwa, mlioyasema yanatoka moyoni, mimi sikupanga kuja hapa, lakini hay ani jambo jema lakini hawa askari wetu ni kama chumvi chumbi kwenye chakula ukiwa hauhitaji, siku chumvi ikipungua mtasema chumvi,” alisema Masauni.

 

Aliwapongeza askari hao kwa kufanya kazi nzuri na amewapa moyo kwa walioyosema wananchji hao, na kuwataka waendelee kufanya kazi nzuri zaidi na kwa uzalendo na Rais Samia yupo pamoja nao katika kuwaboreshea mazingira ya kazi.

No comments:

Post a Comment

Pages