HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 26, 2023

ATCL kuleta Ndege ya Kwanza ya Mizigo, lakutana na Wadau wa Usafirishaji Mizigo

Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam


Katika kukuza huduma zake na kuhakikisha zinaendana na kasi ya ukuaji wa sekta ya usafirishaji wa anga duniani, Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) linatarajia kupokea ndege ya kwanza ya mizigo aina ya Boeing 767-300F yenye uwezo wa kubeba tani 54 mwezi Aprili mwaka huu ambayo itatatua changamoto ya usafirishaji mizigo hapa nchini.

Ujio wa ndege hiyo itakayokuwa mkombozi wa sekta ya usafirishaji mizigo kwa njia ya anga hapa nchini umetangazwa mbele ya wadau mbalimbali na  Msajili wa Hazina Nehemia Mchechu wakati akizungumza na wadau wa Usafirishaji Mizigo, wafanyabiashara pamoja na wawakilishi kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali jamesema kuwa ndege hiyo itaweka historia Afrika Mashariki na nchi Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika, (SADC).

Aidha msajili huyo wa hazina amesema kuwa hapo awali  ATCL ilikuwa ikitumia ndege abiria kusafirisha mizigo japo zilikuwa na uwezo wa kubeba tani chache ukilinganisha na uhitaji wa soko la mizigo,hivyo ujio wa ndege hiyo mpya ya mizigo utamaliza tatizo hilo.

Hata hivyo katika hatua nyingine Mchechu ametoa wito kwa  ATCL kuendelea kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali nchini wakiwemo waagizaji wa mizigo nje ya nchi na ndani ya nchi ili kutatua changamoto zinazokwamisha ufanisi wa biashara hii pamoja na kusimamia maslahi mapana ya pande zote yaani wadau na Serikali.

Kuhusu mahitaji ya soko duniani amesema kwa mujibu wa Ripoti ya Soko la Usafirishaji wa Mizigo ya 2023, ukubwa wa soko la mizigo limekua kutoka $191.01 bilioni mwaka 2022 kufikia $199.09 bilioni kwa mwaka 2023 kwa kiwango cha ukuaji wa kila mwaka (CAGR) cha 4.2% na ukubwa wa soko la usambazaji wa mizigo unatarajiwa kukua hadi $224.78 bilioni mwaka 2027 kwa kiwango cha CAGR ya 3.1%.

Ameongeza kuwa ofisi ya msajili wa hazina itaendelea kutoa ushirikiano kwa shirika hilo ili kuhakikisha linafikia malengo yake pamoja na taasisi na mashirika mengine ya umma.

 

Kwa Upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Mhandisi Ladislaus Matindi amesema kuwa ATCL inajivunia kwa kutoa huduma za uhakika, salama na endelevu za ubora wa juu duniani kote.

Amebainisha kuwa kupitia mkutano huo watachukua maoni kutoka kwa wadau wa usafirishaji mizigo yatakayowezesha kuondoa kero na urasimu kwenye biashara ya Mizigo.

“Yapo mambo yanayotakiwa kufanyiwa maboresho hasa yenye urasimu lakini yapo ambayo ni ufuataji wa sharia za kulinda usalama wa uendeshaji wa biashara hii. Katika kikao hiki wadau watajadili na kukubaliana masuala ya kufanyiwa kazi na kuweka malengo. Lakini pia tutaambizana ukweli kwa wafanyabiashara ambao hawafuati sharia ambazo kimsingi ni kwa faida ya pande zote mbili,” alisema.Imetolewa na Kitengo cha Uhusiano kwa UmmaShirika la Ndege Tanzania (ATCL)." Amesema Matindi

Kwa sasa ATCL ina ndege 12 na imefanikiwa kupanua mtandao wake hadi kufikia vituo 14 vya safari za kitaifa, 8 za kikanda na 2 za mabara.

Nae, Mkurugenzi Mkuu wa kampuni, inayosafirisha mizigo ya maua, matunda, viungo na mbegu, Amani Temu ameishukuru serikali kwa kusikia kilio chao na inaleta ndege ya mizigo.

“Suruhisho la changamoto tuliyokuwa nayo ni hii ndege inayokuja, kwa sisi wadau wa sekta ya usafirishaji tunategemea kuitumi kutokana na wingi wa mizigo na ukuaji wa sekta, tutatumia ndege hii ya mizigo.”

Awali amesema kuwa kulikuwa na changamoto ya ukosekanaji wa nafasi za kusafirisha mizigo kwenye ndege hasa katika kipindi ambacho kunakuwa hakuna abiria wengi kwa sababu tulikuwa tunategemea ndege za abiria na upatikanaji wa nafasi ya mizigo unakuwa mdogo.

No comments:

Post a Comment

Pages