HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 08, 2023

MST yashauri Afya Bora ya Uzazi kwa Wanawake Wote

Na Irene Mark

WAKATI Dunia ikiadhimisha Siku ya Wanawake leo Machi 08,2023 Shirika la Maria Stopes Tanzania (MST), limeishauri Serikali na wadau kuwekeza zaidi kwenye huduma borabna taarifa sahihi za afya ya uzazi.

Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Marie Stopes Tanzania, V.S Chandrashekar alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mchango wa MST kwa ushirika na serikali katika kutoa taarifa sahihi na huduma bora za afya nchini.



Alisema huduma bora na taarifa sahihi za afya ya uzazi ni muhimu kwani taifa litakuwa na wanawake na wasichana wenye uwezo wa kuamua jambo sahihi kuhusu masuala yao ya afya ya uzazi.

“Hii pia itasaidia serikali kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) manne kwa wakati mmoja ambayo ni lengo namba tatu afya njema na ustawi, lengo namba nne elimu bora, namba tano usawa wa jinsia na la nane ni kazi nzuri na ukuaji wa uchumi,” alisema Chandrashekar.

Alisema pia kuna haja ya serikali kupitia sera na sheria zenye vikwazo zinazoathiri njia za muda mfupi za uzazi wa mpango kama vile upatikanaji wa kondomu na upatikanaji wa vidonge vya dharura vya kuzuia mimba kwenye kaunta na utoaji wa dawa kupitia vituo vilivyoidhinishwa vya kusambaza dawa.

Pamoja na hayo mkurugenzi huyo alieleza kuwa shirika hilo la MST kwa kushirikiana na serikali na wadau wengine kwa mwaka 2022 limefanikiwa kusaidia zaidi ya wateja milioni 1.6 kupata elimu na huduma za afya ya uzazi ikiwa ni ongezeko la asilimia 27 ikilinganishwa na mwaka 2021.

Alisema katika eneo la uzazi wa mpango shirika hilo lilitoa huduma kwa watu milioni 4.7 ongezeko la asilimia 29 ikilinganishwa na mwaka 2021 na ni sawa na asilimia 40 ya huduma za uzazi wa mpango zilizotolewa nchini.

Kwa mujibu wa Chandrashekar huduma hizo zimesaidia kuokoa mimba zisizotarajiwa milioni 1.67, vifo vya uzazi 2,947 na utoaji mimba usio salama 412,000.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Afya wa MST Dk Geofrey Sigalla alisema shirika hilo pia kwa mwaka jana limetoa huduma ya uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake 12,420, limesaidia waathirika wa ukatili wa kijinsia 14,032 na kupima VVU na ushauri kwa watu 10,570.

“Shirika pia limeshirikiana na serikali kuwajengea uwezo watoa huduma wa serikali katika mikoa ili kutoa huduma za afya zenye ubora unaotakiwa. Limetoa vifaa vya kutolea huduma katika mikoa na kuwajengea uwezo waelimishaji rika na jamii kuhakikisha wanatoa taarifa sahihi kuhusu afya ya uzazi,” alisema Dk Sigalla.

No comments:

Post a Comment

Pages