Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimedhatiti katika kuzalisha wataalamu wazalendo watakaosaidia kuleta maendeleo nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ametoa kauli hiyo uzinduzi wa kituo cha utafiti wa Bahari, mazingira na Maliasili uliofanyika viwanja vya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kampasi ya Betrasi Mkoa wa Mjini wa Magharibi.
Amesema dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Dkt. Hussein Ali Mwinyi ni kuhakikisha wataalamu wanapata ujuzi utakaotumika katika kuratibu na kushajihisha matumizi ya Sayansi na Teknolojia jambo ambalo litapelekea Taifa kuwa na maendeleo ya haraka ya kijamii na kiuchumi.
Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya nane imetilia mkazo Sera ya Uchumi wa Buluu ili kuongeza pato la Taifa na kuinua hali za wananchi kiuchumi ambapo moja kati ya mihimili ya Uchumi wa Buluu ni uvuvi ambao unahusisha ufugaji wa mazaoya baharini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema uanzishwaji wa kituo cha utafiti wa Bahari, mazingira na Maliasili unaunga Mkono juhudi za Serikali na unaenda na Azma na sera ya pamoja katika kuimarisha Uchumi wa Buluu.
Aidha Mhe. Hemed amesisitiza kuwa kituo hicho ni vyema kifanye tafiti zenye tija kwa wananchi ili kutoa suluhisho la matatizo wanayokumbana nayo katika shughuli zao za ufugaji wa samaki.
Pamoja na hayo Mhe. Hemed ameupongeza Uongozi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha (SUZA) kwa kuanzisha kituo hicho hatua ambayo inatia moyo juu ya kuleta Mabadiliko ya Kiuchumi Zanzibar kupitia Sekta ya Uchumi wa Buluu.
Vile vile amewapongeza wataalamu na watafiti wazawa waliobuni na kusimamia Mradi huo ambao watasaidia kwa kiasi kikubwa kivitendo katika kuimarisha Uchumi wa Zanzibar.
Aidha Mhe. Hemed ameupongeza Uongozi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia Tanzania ( COSTECH) kwa kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuinua sekta ya Buluu.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Profesa Moh'd Makame Haji ameishukuru Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia kwa kuwaandalia miundombinu ya tafiti hizo zenye mchango mkubwa wa kusimamia Sera ya Uchumi wa Buluu nchini.
Amesema Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kinaenda sambamba na azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kukuza ustawi wa wananchi wake.
Nae Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH) Dkt. Amos Nungu amesema Mradi huo unatokana na ushindani uliohusisha Taasisi za Kitaaluma na kujumuisha Maandiko sabini na Tano (75) na andiko la Chuo kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) lilishinda Shindano hilo ambapo wanaamini Chuo hicho kina uwezo mkubwa wa kufanya tafiti mbali mbali zinazohusu sayansi ya bahari na kuahidi kuendelea kuunga Mkono tafiti hizo.
No comments:
Post a Comment