Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO
Serikali
imedhamiria kupunguza gharama za kusafisha figo kutoka Shilingi 350,000
mpaka Shilingi 90,000 hadi 150,000 kwa lengo la kuwapunguzia wananchi
mzigo wa gharama za matibabu hasa kwa wenye vipato vya chini.
Taarifa
hizo zimetolewa leo bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Wizara ya
Afya, Mhe. Dkt. Godwin Mollel wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti
Maalum kupitia Vijana, Mhe. Lucy Sabu lililohoji kuhusu mpango wa
Serikali kupunguza gharama za kusafisha figo.
Naibu
Waziri Mollel amesema kuwa, Serikali imekuwa ikitoa huduma za matibabu
ikiwemo huduma ya kusafisha figo kwa wagonjwa wote bila kujali kipato
cha mgonjwa husika ambapo huduma hizo kwa sasa zinatolewa katika
Hospitali ya Taifa Muhimbili, hospitali za Rufaa za Kanda, Mikoa na
Hospitali Maalum ikiwemo Hospitali ya Chuo Kikuu cha Dodoma.
"Katika
eneo la huduma za kusafisha figo, wizara imegundua kuna uwezekano wa
kupunguza gharama za huduma hiyo badala ya kuwa 350,000 kwa awamu moja,
mgonjwa ataweza kutibiwa kwa gharama ya kuanzia 90,000 hadi 150,000 kwa
awamu moja, hivyo kuna mpango wa kushusha gharama hizo, amesema Naibu
Waziri Mollel.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi
wenye kipato kidogo kufuata taratibu zinazopelekea wao kupata misamaha
ya huduma (exemption) ikiwemo huduma hii ya usafishaji wa figo kwa
kuwasilisha barua kutoka kwa Mtendaji wa Kata husika.
Vile
vile, Naibu Waziri Mollel amejibu swali la Mbunge wa Viti Maalum
kupitia Kundi la Asasi za Kiraia Tanzania (NGOs), Mhe. Neema Lugangira
lililohoji kuwa Serikali imefikia wapi katika kufanya tafiti kwenye
mikoa ya Kanda ya Ziwa ili kubaini sababu zinazopelekea kuwa na wagonjwa
wengi wa Kansa za aina mbalimbali ambapo alifafanua kuwa, zaidi ya
Sampuli 700 za wananchi wanaoishi Kanda ya Ziwa zimekusanywa kwa ajili
ya kupelekwa kufanyiwa uchunguzi ili kubaini chanzo cha kukithiri kwa
ugonjwa wa Kansa katika maeneo hayo.
"Baada ya
kukusanya sampuli hizo na kuzipeleka maabara, hatua tuliyoifikia kwa
sasa ni kuzichambua sampuli hizo kwenye kiwango cha vinasaba ili tuweze
kuona tatizo au sababu ya maeneo hayo kuathirika zaidi na ugonjwa huo,"
amesema Dkt. Mollel.
No comments:
Post a Comment