Na Mwandishi Wetu
MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, amesema Mradi wa Maji unaotekelezwa katika ya Same na Mwanga utamaliza tatizo la uhaba wa maji katika wilaya hizo kabla ya Mwaka 2024.
Babu amesema hayo wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Same na kuwataka madiwani wa halmashauri hiyo kueneza taarifa hizo kwa wananchi ili waweze kufahamu hatua zilizochukuliwa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
"Mama yetu Mheshimiwa Rais Samia ametoa fedha nyingi kuhakikisha Mradi wa Maji Same, Mwanga na Korogwe unakamilika kwa wakati kuwawezesha wananchi kunufahika na maji safi na salama," alisema.
Alisema kazi kubwa ya madiwani ni kumsaidia Rais Samia katika utekelezaji wa miradi na kuwaelimisha wananchi kufahamu faida ya miradi inayotekelezwa katika maeneo yao.
Mbali na hayo Babu amewataka madiwani kushirikiana kikamilifu katika kutoa elimu kwa wananchi na pia kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuleta maendeleo.
No comments:
Post a Comment