HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 15, 2023

*MwaFA apongezwa kwa kazi anazozifanya jimboni*


Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe Hamisi Mwinjuma maarufu MwanaFA akizungumza na wana-CCM wa kata ya Kwafungo.


Katibu wa Mwenezi wa CCM Wilaya ya Muheza ndugu Mwedi. 


Diwani wa Kata ya Kwafungo Gabriel Mathayo Mswagala akitaja kazi zilizofanywa na mbunge wao.


Na Mashaka Mhando, Muheza


MADIWANI wa kata za Bwembwera na Kwafungo, wamesifu kazi nzuri za miradi ya Maendeleo zilizofanywa na Mbunge wa jimbo la Muheza Hamisi Mwinjuma maarufu MwanaFA.


Wakitoa pongezi hizo kwa nyakati tofauti kwa mbunge huyo ambaye ni Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, diwani wa kata ya Bwembwera Ally Nyangasa, alisema kwa miaka miwili wamepiga hatua kubwa katika miradi ya elimu, afya na maji.


"Umetuletea shilingi milioni 30 tukajenga maabara katika shule yetu ya sekondari, milioni 20 tukajenga darasa, ukaleta tena milioni 12.5 na mifuko 80 ya saruji tukajenga darasa la kisasa kule Msowelo," alisema diwani huyo.


Alisema katika kijiji cha Mkuyuni Bwembwera walipata shilingi milioni 12.5 na mifuko 20 ya saruji kujenga darasa na pia walipewa shilingi milioni 2 kwa ajili ya kujengwa choo katika shule ya msingi Mamboleo lakini pia mbunge huyo alitoa pump mpya ya maji ya kisima katika kijiji hicho.


"Muheza hatuna sababu ya kutafuta mbunge mwingine mwaka 2025 mbunge wetu utakuwa wewe, tupelekee salamu zetu kwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan mwambie tunampenda kwa upendo wake kwetu kupitia wewe mwakilishi wetu," alisema diwani huyo.


Diwani wa kata ya Kwafungo Gabriel Mathayo Mswagala, amemhakikishia mbunge wa jimbo hilo kwamba alale usingizi ifikapo mwaka 2025 pamoja na Rais Dkt Samia kwa vile kazi walizozifanya hawana budi kuwalipa kwa kuwapa kura za kutosha.


"Mheshimiwa mbunge, mwaka 2020 hatukuunga mkono katika kura za maoni ndani ya chama chetu lakini mwaka 2025 tutakuunga mkono kwenye kura za maoni kutokana na kazi zako ulizotufanyia kwa miaka hii miwili," alisema diwani huyo.


Diwani huyo aliainisha kazi mbalimbali alizofanya mbunge huyo katika vijiji vinne vilivyopo katika kata hiyo ikiwemo ujenzi wa kituo cha afya ambacho kimejengwa katika kijiji cha Bagamoyo na walipokea shilingi milioni 500 za awamu ya kwanza.


Alisema amewachimbia visima virefu vya maji amewapa shilingi milioni 12.5 kujenga darasa shule ya msingi Kwafungo lakini pia ametoa kiasi cha shilingi milioni 80 kujenga madarasa manne shule ya sekondari Kwafungo.


Diwani huyo aliongeza kusema kwamba pia mbunge amewatengenezea karavati na kukarabatiwa barabara ya iliyokuwa korofi ya kutoka Kwafungo-Mbambara-Mtindiro hadi Kilulu ambayo pia barabara hiyo diwani huyo alimuomba mbunge aipiganie iingie kwa Wakala wa barabara nchini (Tanroad).


Pia alisema mbunge wao hakuishia hapo, amewapa shilingi milioni 1.3 kutengeneza madawati lakini pia kijiji cha Mandela ametoa shilingi milioni 2.5 kujenga madarasa mawili ya shule ya msingi katika kijiji hicho na kitongoji cha Mahanji kimepatiwa umeme.


Alisema katika kijiji cha Mbambala walipewa shilingi milioni 40 kujenga madarasa mawili na milioni 61 kujenga nyumba ya walimu.


"Mheshimiwa mbunge wetu watakaokuja waacheni waje lakini kwa kazi hizi ulizotufanyia tutakuwa watu wa ajabu sana kama hatutakuchagua," alisema na kuongeza,


"Sisi imani yetu tumeiweka kwako wanaopita waache wapite lakini tutakupa kura za mafuriko, hatuwezi kukuacha wewe Naibu Waziri tukamchagua mtu mwingine hatuna uenda wazimu huo,".


Akizungumza katika kata hizo mbunge huyo, aliwapa salamu wananchi kutoka kwa Rais na kamba ushindi walioupata Julai 13 mwaka huu wa udiwani kata ya Potwe.


Pia alisema kuwa katika kipindi cha miaka miwili akiwa mbunge wilaya hiyo imepata miradi mingi kuliko kipindi kingine chochote kile hivyo aliwataka Wana-CCM kitembea kifua mbele kama wamepigwa ngumi za mgogo.


"Wilaya yetu ya Muheza tangu ianzishwe mwaka 1974 ikiwa ni miaka 46 imenizidi umri lakini hakuna kipindi ambacho tumepata miradi mingi kuliko kipindi kingine chochote kile hivyo tumuungeni mkono Rais wetu," alisema.


Alisema hataki ifikapo mwaka 2025 Muheza iwe vile alivyoikuta wakati akiingia ambapo kwa miaka mitano iliyopita alikuta wamejenga madarasa 20 tu wakati wao hadi sasa tayari wamejenga madarasa 169 kupitia Rais Dkt Samia.


"Siyo mtuunge mkono kwasababu ni mwenzenu wa CCM, tunataka mtuunge mkono kwasababu kazi imefanyika," alisema na kuongeza,


"Nataka niwahakikishie tumefanya vizuri kuliko kipindi chochote kile hivyo tembeeni kifua mbele kama mmepigwa ngumi ya mgongo," 


Aliwataka Wana-CCM kumsemea vizuri Rais, Mbunge, diwani na CCM ambapo serikali imetekeleza kwa vitendo kazi ilizoziahidi kwenye ilani ya chama.


Aliwaahidi kwamba atatekeleza ahadi zote ambazo alizitoa wakati wa kampeni ikiwemo suala la kumalizia vitongoji 60 ambavyo havina umeme.

No comments:

Post a Comment

Pages