Na Ashraq Meraji, Hai
MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amepongeza wananchi wa kata ya Muungano, tarafa ya Masama wilayani Hai kwa usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Babu ametoa pongezi hizo wa ziara ya kikazi aliyofanya katika wilaya hiyo kwa ajili ya ukaguzi wa ujenzi wa shule mpya ya Msingi Mlima Shabaha yenye jumla ya vyumba tisa vya madarasa, jengo la utawala, matundu 16 ya vyoo pamoja na kichomea taka inayotekelezwa na Mradi BOOST
Alisema ujenzi huo ambao umegharimu shilingi milioni 348.5 ni ushishidi tosha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kumkomboa mtoto wa kitanzania katika elimu.
“Nitoea pongezi kwa uongozi wa Hai chini ya Mkuu wa Wilaya Amir Mkalipa kwani inaonekana wazi kuwa wamesimamia ujenzi vizuri, nataka maeneo mengine ambayo miradi mikubwa kama hii inatekelezwa usimamizi uzingatiwe,” alisema.
Alisema dhamira ya serikali ni kuhakikisha watoto wa kitanzania wanapata elimu katika mazingira mazurim, hivyo itakuwa jambo la aibu iwapo kuna watumishi watashindwa kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Babu alisema Serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria pale ambapo watabaini uwepo wa watendaji ambao wanatumia fedha za miradi vibaya.
Kwa upande wake Mkalipa alisema shule hiyo inaenda kuwa mkombozi wa wanafunzi waliokuwa wakitembea umbali mrefu zaidi ya kilomita mbili kufuata elimu na pia itawalinda wanafunzi wasifanyiwe vitendo viovu na wapita njia.
Mkalipa ametoa pongezi zake kwa Rais Samia na Serikali kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo na miradi mingine ya maendeleo inayotekelezwa wilayani hapo.



No comments:
Post a Comment