Timu kuanza kutua Moro kesho
JOTO la mashindano ya Riadha ya Taifa 2023 yanayotarajiwa kufanyika kwa siku mbili mkoani Morogoro kuanzia Septemba 29 hadi Septemba 30, limezidi kupanda ambapo mikoa shiriki imeanza kuwasili mjini humo.
Jumla ya washiriki 207 wanatarajiwa kushiriki mashindano ya mwaka huu.
Kwa mujibu wa Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Wakili msomi Jackson Ndaweka, mikoa 31 ya Tanzania Bara na Zanzibar inatarajiwa kushiriki.
Wakili Ndaweka, alisema mashindano hayo ni muhimu kwa mustakabali wa mchezo wa Riadha, hasa ukizingatia mwakani kutakuwa na matukio mengi makubwa kimataifa.
Kwa mujibu wa orodha maalumu iliyotolewa, mikoa ya Kusini Unguja, Arusha, Kilimanjaro na Dar es Salaam itatoa wachezaji 15 na viongozi wawili kila mmoja.
Mikoa inayofuatia ni Singida, Tanga na Tabora yenye wachezaji 10 kila mmoja na viongozi wawili.
Mkoa wa Kaskazini Unguja wachezaji saba, Mjini Magharibi sita huku Kaskazini Pemba na Kusini Pemba ikiwa na wachezaji watano kila mmoja na kiongozi mmoja.
Mikoa mingine yote iliyosalia imepewa nafasi ya wachezaji wawili na kiongozi mmoja kila mmoja, isipokuwa mwenyeji Morogoro ambaye yuko huru kwa idadi ya washiriki.
Awali, RT iliitaka mikoa kuendesha mashindano ya majaribio na kutuma matokeo kwenye shirikisho, kwani ndio itakuwa moja ya kigezo cha ugawaji kota.
Mashindano hayo yanakuja ikiwa ni kiu ya muda mrefu ya mikoa, hivyo yanatarajiwa kuwa na ushindani wa hali ya juu.
No comments:
Post a Comment