Mbunge wa Viti Maalum Neema Lugangira akigawa mitungi ya gesi kwa wakina mama wa wajasiriamali Wilaya ya Bukoba Mjini mkoani Kagera.
Na Mwandishi Wetu
MBUNGE wa Viti Maalum Neema Lugangira amezindua Kampeni ya "Pika kwa Gesi, Tunza Mazingira" inayolenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ambapo amegawa mitungi 300 ya gesi.
Lugangira amezindua kampeni hiyo Septemba 14,2023 wilayani Bukoba mkoani Kagera ambapo ameweka wazi kuwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo aliyotoa Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa Kongamano la Nishati Safi ya Kupikia lililofanyika Novemba Mosi 2022, mkoani Dar es Salaam.
Mbunge huyo amesema kuanzia ametoa mitungi 300 ya gesi kwa viongozi wa makundi mbalimbali, wajasariamali, mama lishe na Wwatu mashuhuri katika Wilaya ya Bukoba mjini mkoani humo.
Amesema Kampeni ya Pika kwa Gesi, Tunza Mazingira imeanzishwa na kuratibiwa na ofisi yake kupitia Neema na Maendeleo na Shirika la Agri Thamani.
"Kampeni hii imeanzia Wilaya ya Bukoba ikifuatiwa na Wilaya ya Muleba na baadae itafika maeneo mengine ndani na nje ya Mkoa wa Kagera kulingana na uwezeshwaji utakaopatikana," amesema.
Mbunge Lugangira ameishukuru Wizara ya Nishati kwa kuwapa semina wabunge kuhusu umuhimu wa kuhamasisha nishati safi ya kupikia na uwezeshwaji uliofanikisha uzinduzi huu.
Aidha, Lugangira ameshukuru Jamilla Haroub, Mratibu wa REA Bukoba na Masota Mafuru, Ofisa Masoko Oryx Gas Mkoa wa Kagera na Geita kwa ushirikiano mkubwa waliompatia.
Mbunge huyo ambaye amekuwa akipambana kutatua changamoto za jamii, amewakaribisha wadau wengine kumuunga mkono kufanikisha Kampeni ya Pika kwa Gesi, Tunza Mazingira ili kuweza kufikia makundi mengine kwenye jamii kwa lengo la kulinda afya za wakina mama, kutunza mazingira na kuepusha madhara ya mabadiliko ya tabia nchi, mambo ambayo yatapelekea kuimarisha lishe bora.
No comments:
Post a Comment