Ushiriki wa Tanzania katika Maonesho ya 68 ya Vito na Usonara katika jiji la Bangkok nchini Thailand umewavutia Wafanyabiashara mbalimbali wa madini kutokana na wengi kutumia malighafi za madini kutoka nchini.
Akizungumza
baada ya kushiriki hafla fupi ya ufunguzi wa maonesho hayo, Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo amesema wafanyabiashara
wakubwa wa madini nchini humo wakiwemo viongozi wa Serikali wameonesha
nia ya kushirikiana na Tanzania katika nyanja mbalimbali zikiwemo
biashara ya madini, uongezaji thamani madini pamoja na kubadilishana
uzoefu katika shughuli hizo.
Aidha, Mbibo amesema uwepo wa
Tanzania katika maonesho hayo ya madini yenye thamani kubwa unalenga
kujifunza pamoja na kuhamasisha urejeshwaji wa minada ya madini nchini
na kuhamasisha uwepo wa masoko ya madini ambapo wafanyabiashara hao
wanaweza kununua madini kupitia masoko ya madini yaliyoanzishwa katika
kila mkoa nchini.
Serikali kupitia Wizara ya Madini inatarajia
kurejesha tena minada ya madini nchini pamoja na Maonesho ya Kimataifa
ya Vito na Usonara ya Arusha yatakayofanyika kila mwaka kulingana na
kalenda za kimataifa ya maonesho ya madini ya vito na biashara za
usonara.
Aidha, hivi karibuni Serikali kupitia Tume ya Madini
ilitoa taarifa kuwa, Wizara ipo kwenye mchakato wa kuwasilisha
mapendekezo ya maboresho ya Sheria na Kanuni ili kuwezesha maonesho na
minada ya vito kufanyika nchini ikiwemo marekebisho ya Kanuni za Eneo
Tengefu la Mirerani za Mwaka 2021 ambazo zilizuia kuuzwa kwa madini ya
Tanzanite nje ya Mirerani.
Kufuatia hayo, Mbibo ametoa wito kwa
wauzaji, wachimbaji, waongezaji thamani madini kutumia uhusiano mzuri
uliopo kati ya Tanzania na Thailand ambao umekuwepo kwa muda mrefu
kuchangamkia fursa hiyo ikiwemo kuungana na wadau wa nchi hiyo katika
masuala yanayohusu mnyororo wa shughuli za madini.
Ameongeza
kwamba, tayari Serikali ya Awamu ya Sita imefungua milango ya biashara
katika Sekta ya Madini na kuwataka wadau wa madini nchini kutumia fursa
hiyo kuwapokea wawekezaji mbalimbali ili hatimaye kujenga uchumi imara
na kuinua ustawi wa watanzania kupitia rasilimali madini.
‘’Biashara
lazima iwe na wauzaji na wanunuzi wawe tayari kupokea watu wengine na
wajifunze namna ya kufanya biashara kutoka biashara ya kitaifa hadi
kimataifa kwa madini ya thamani na mawe,’’ amesema Mbibo.
Akizungumza
baada ya ujumbe wa Tanzania kutembelea banda la Kampuni ya Bright
Future katika maonesho hayo, Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Ashish Baid
ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Shirikisho la Wafanyabiashara wa
Madini nchini humo na mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite na madini
mengine, ameelezea nia yake ya dhati kupitia jukwaa hilo na kampuni
yake binafsi ya kushirikiana na Tanzania katika kuipa thamani ya
kimataifa minada ya madini endapo Serikali itakuwa yatari kushirikiana
nao ikiwemo katika eneo la uongezaji thamani madini.
Ameongeza
kwamba, kwa kuzingatia uhusiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na
Thailand na kutokana na utajiri wa rasilimali madini zilizopo nchini
ikiwemo madini pekee ya Tanzanite, wananchi wa Tanzania na taifa hawana
budi kunufaika ipasavyo na rasilimali hiyo na si kwa wafanyabiashara
pekee wa madini na kuongeza,’ ’ikiwa sisi wafanyabiashara tunanufaika
ni muhimu sana Kwa Tanzania kunufaika," amesema.
Naye, Mkurugenzi
wa Masoko wa Kampuni ya Fine Gamestone Sukharit Sinchawla baada ya
kutembelewa na ujumbe wa Tanzania amesema amefurahishwa na uwepo wa
Tanzania katika maonesho hayo na kusema ni nchi nzuri yenye madini
mengi mazuri na yenye thamani kubwa na kueleza kwamba ni nchi ambayo
kampuni yake inatumia madini mengi kufanya biashara yakiwemo ya Spinel
na Tanzanite.
Maonesho ya BangKok ni moja ya maonesho ya madini
ya vito na usonara maarufu zaidi duniani na yamekuwepo nchini humo kwa
miaka mingi. Maonesho hayo yameandaliwa na Idara ya Ukuzaji Biashara ya
Kimataifa ya Thailand.
Aidha, biashara ya madini nchini humo imetajwa kuwa ya pili katika kuchangia fedha za kigeni ikiwemo kukuza ajira .
Wadau
muhimu wapatao 31 elfu kutoka maeneo mbalimbali duniani wanatarajia
kutembelea maonesho hayo kutoka nchi 21 na waoneshaji takribani
1,100.
Imeelezwa kuwa mwaka 2022 mauzo ya vito na usonara nchini
humo yalifikia thamani ya Dola za Marekani milioni 800 na mwaka huu
mauzo yanatarajiwa kufikia Dola za Marekani milioni 850.
Maonesho
ya BangKok ni maonesho makubwa na ya kuaminika ambayo wafanyabiashara
wachimbaji wanaweza kuyatumia kujenga uhusiano wa kibiashara, kutangaza
bidhaa zao na kuuza.
Mbali na Naibu Katibu Mkuu, wengine
wanaoshiriki ni wawakilishi kutoka Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati
na Madini, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Wataalam kutoka
Wizara ya Madini na Tume ya Madini.
No comments:
Post a Comment