Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia na kuwahoji kwa kina askari wa Kampuni ya Ulinzi PASCO LTD 11, Maafisa wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) wawili na askari Polisi 6.
Akizungumza na wanahabari Jijini Dar es Salaam Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam SACP Muliro Jumanne Muliro amesema Agosti 29, 2023 Majira ya saa 8 (nane) usiku eneo la Kiluvya Ubungo, maafisa kutoka katika taasisi hizo wanadai wakati wa utekelezaji wa majukumu yao, lilitokea kundi la watu wanaokadiriwa kuwa 30 wakiwa na pikipiki zilizokuwa zimebeba magunia ya mkaa ambayo ni mazao ya misitu na walipofika eneo la ukaguzi na kuamriwa wasimame, walikaidi na kuanza kufanya fujo.
Katika fujo hizo waliwarushia mawe Maofisa wa maliasili na wenzao wakishinikiza pikipiki zilizo kuwa na mkaa kinyume na sheria ziachiwe.
Aidha Mafisa wa timu hiyo waliokuwa na silaha walianza kufyatua risasi kwa lengo la kuwatawanya na kujilinda.
Hata hivyo ilibainika kuwa watu wawili walijeruhiwa katika purukushani hizo na walipoteza maisha baada ya kufikishwa hospitali ya Mloganzila.
Ameongeza kuwa katika tukio hilo Pikipiki 16 ambazo zilitelekezwa na watu hao na magunia ya mkaa vilipelekwa Mpingo House.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum linachunguza mazingira yote ya tukio hilo kwa kushirikiana na mamlaka zingine za kisheria na halitasita kuwachukuliwa hatua zingine za kisheria kulingana na sheria za Nchi.
Hata hivyo amesema Watu waliokuwa kwenye kazi hiyo wako chini ya ulinzi na silaha zao zimepelekwa kwenye mamlaka za kiuchunguzi za silaha/bunduki Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Mloganzila kwa uchunguzi.
No comments:
Post a Comment