NA MAGENDELA HAMISI
BAADHI ya wanasiasa na wanaharakati nchini wametakiwa kuacha uchochezi ambao unaweza kuvuruga amani ya nchi na wakitakiwa kutumia vizuri fursa ya kufanya mikutano ya kisiasa ambayo imetolewa na Rais, Dkt Samia Suluhu Hassan ili kudumisha utamaduni wa utulivu wa Watanzania.
Hayo yamebaishwa leo Septemba 13, 2023 jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Taasisi ya ‘Team Wazalendo’, Frank Rugwana wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amewasisitiza wanasiasa na wanaharakati kujikita katika kutoa hoja za msingi na si kutukana au kusema uongo ili wapate wafuasi wa kuwaunga mkono.
“Baada ya Rais wetu mpendwa kutoa ruhusa ya kufanya mikutano ya kisiasa iliyokuwa imepigwa marufuku hadi zitakapowadia chaguzi, tayari baadhi ya wanasiasa wameanza kufanya siasa chafu, kusema uongo na kufanya uchochezi mambo ambayo yanaweza kuhatarisha amani ya nchi yetu kama hatutakemea.
“Tunawaomba wanasiasa hao kuacha mara moja kufanya siasa chafu zinazoweza kuleta machafuko kwa maana wapo baadhi ya watanzania wasiokuwa na chama chochote cha siasa ikiwa yatatokea machafuko watakuwa wameonewa jambo ambalo litatufanya tujisikie uchungu na hatutaki kuona likitokea,” amesema.
Ameongeza kuwa ikiwa wanasiasa hao wataendelea kufanya uchochezi na kusema uongo kwenye mikutano yao ya kisiasa ili kutimiza malengo yao ovu ya kuwagawa Watanzania, taasisi hiyo itataja vikao vyao pamoja na makundi yanayofadhiri mkakati huo.
Amesema kuwa Watanzania hawana utamaduni wa kuchukiana au kukosa kueleawana, misingi ya amani ambayo ipo nchini inajengwa vema na kuelewana, maridhiano, mshikamano, upendo, umoja na kujisahihisha kwa viongozi.
Rungwana, amefafanua kuwa katika kujisahihisha kwa viongozi, Dkt Samia akiwa ni kiongozi wa nchi amefanikisha kufuta kesi zote za uzushi kwa wanasiasa waliobambikiwa na katika dhamira njema aliyokuwa nayo amefungua mlango wa maridhiano kwa wanasiasa ili kuendeleza kuweka ustawi mzuri wa taifa na kuruhusu mikutano ya hadhara iliyokuwa imezuiwa.
Pia amerejesha mchakato wa Katiba Mpya jambo lililokuwa kiu kwa wanasiasa na baadhi ya watanzani, katika kuonesha upendo ametafuta fursa za kiuchumi kwa maslahi mapana ya watanzania katika kipindi cha uongozi wake tangu aingie madarakani, hivyo anapaswa kupongezwa.
“Tunatoa rai kwa watanzania kukemea tabia za baadhi ya wanasiasa wanaochochea uovu , tusipokemea taifa letu linaweza kuingia katika machafuko jambo ambalo hatutaki kusikia wala kuona, ebu angalia baadhi ya nchi ambazo zimeingia kwenye machafuko namna wanavyotaabika,ukichunguza nyuma kulikwa na wanasiasa wachochezi na baada ya hapo wanatoroka nchi na kuacha taifa likiangamia, shime watanzania tuwapuuze wanasiasa wenye mlengo wa kutugawa, sisi ni wamoja , tubaki kuwa wamoja hadi mwisho wa dunia, hakuwa wa kutugawa, tusimame imara kuitetea nchi yetu na viongozi wetu” amesema.
No comments:
Post a Comment