Kampuni ya Qwihaya General Enterprises LTD ya mjini Mafinga Mkoani Iringa imetoa msaada wa vipande vya mbao
2,200 vya kupaulia kwa ajili ya kujenga upya makazi yao.
Msaada
huo umetolewa ikiwa na Lengo la kurejesha tabasamu miongoni mwa wakazi
zaidi ya 350 kutoka kaya 50 za mitaa ya Buganda na Ilemela Mahakamani
Manispaa ya Ilemela ambao nyumba zao zilibomolewa kwa mvua iliyoambatana
na upepo mkali.
Msaada huo wenye thamani ya
zaidi ya Sh13.2 milioni umekabidhiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni
ya Qwihaya, Benedicto Mahenda Qwihaya ikiwa ni kuitikia wito wa Serikali
kwa wadau kujitokeza kusaidia waathirika kujenga upya makazi yao baada
ya janga hilo lililotokea Septemba 6, mwaka huu.
Kupitia
msaada huo, kaya 16 za Mtaa wa Buganda ambao nyumba zao zilibomoka
kabisa zimepata vipande 47 vya mbao huku kaya nyingine 13 ambazo nyumba
zao hazikupata madhara makubwa zikipewa mbao 30 kila moja.
Msaada
kama huo pia umetolewa kwa Kaya 21 kutoka Mtaa wa Ilemela Mahakamani
ambao pia waliathiriwa na mvua hizo zilizowaacha wananchi wakilala nje
kwa kukosa makazi.
Akikabidhi msaada huo,
Mkurugenzi wa Qwihaya, Benedicto Mahenda amesema uongozi wa kampuni hiyo
inayojihusisha na biashara ya mazao ya misitu uliguswa na taarifa za
janga hilo zilizotangazwa kupitia vyombo vya habari ikiwaonyesha watoto,
wazee na wanawake wakiwa wamelala nje kwa kukosa makazi baada ya nyumba
zao kubomolewa.
“Tumetoa sehemu kidogo ya tulichojaaliwa na Mwenyezi Mungu kusaidia waathirika kujenga upya makazi yao,’’ amesema Mahenda
Akishukuru
kwa niaba ya wenzake, Regina Chrisant, mmoja wa waathirika, mkazi wa
Mtaa wa Buganda ameishukuru kampuni ya Qwihaya, Serikali na wadau wote
kwa misaada inayowawezesha kurejea katika maisha yao ya kawaida baada ya
janga lililowaacha wakiwa hawana makazi.
‘’Misaada
hii ya hali na mali imeturejeshea matumaini siyo kwa kwa kutuwezesha
kuyajenga upya makazi yetu, bali pia inaonyesha jinsi Watanzania
tunavyoishi kwa upendo miongoni mwetu,’’ amesema Regina
Stanslaus
Francis, mwathirika mwingine aliyepokea msaada ameomba wadau zaidi
kujitokeza kusaidia waathirika kurejea katika maisha yao ya kawaida
baada ya janga hilo ambalo alikusababisha majeruhi wala vifo.
Shukrani
zingine zimetolewa na Diwani wa Kata za Shibula iliko Mtaa wa Buganda,
Swila Dede (CCM) huku akiwaomba wadau wengine kujitokeza kuitikia wito
wa Serikali wa kusaidia wananchi kwa sababu bado kuna mahitaji mengi
ikiwemo ya chakula, samani za ndani na vifaa vingine vya ujenzi.
Mwenyekiti
wa Serikali ya Mtaa wa Buganda, Evarsit Chikanga amewataka wanaopokea
msaada kuitumia kwa malengo mahusui ikiwemo kujenga upya makazi yao huku
Mratibu wa Maafa Manispaa ya Ilemela, Jamses Wembe akiwataka wananchi
wanaoishi jirani na fukwe na wanaofanya shughuli za kiuchumi na kijamii
ndani ya Ziwa Victoria kuchukua tahadhari mvua na upepo mkali.
Kwa
mujibu wa Wembe, tahadhari hiyo inatokana na utabiri iliyotolewa na
Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) kuhusu uwezekano wa ukanda wa Ziwa
Victoria kupata mvua nyingi utakaoambatana na upepo mkali ndani ya siku
tano zijazo.
No comments:
Post a Comment