Mwandishi Wetu, Mugumu
Wajumbe wa Hifadhi ya Jamii ya Burunge WMAs ya Wilaya ya
Babati,mkoa wa Manyara wamekubaliana
kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri na serikali kusimamia masuala ya uhifadhi ikiwemo ulinzi
wa Shoroba.
Uamzi huo umefikiwa leo Jumatatu Desemba 18,2023 katika kikao cha pamoja kwenye ukumbi wa Kampango Hotel Mugumu Serengeti,ikiwa ni sehemu ya ziara ya viongozi hao, kutembelea jumuiya ya hifadhi ya jamii ya Ikona, kujifunza jinsi ya kukabiliana na migogoro baina ya wanyamapori na binaadamu.
Viongozi wa Burunge WMA wakiwepo Wajumbe wa kamati ya uongozi(AA), wajumbe wa Bodi na viongozi wa halmashauri ya Babati na idara ya wanyamapori mkoa Manyara,wanafanya ziara ya mafunzo Ikona WMA, ziara ambayo inafadhiliwa na taasisi ya chemchem Association, ambayo imewekeza shughuli za uhifadhi na Utalii katika eneo hilo,
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Anna Mbogo amesema,ili kuhakikisha ziara ya viongozi hao wa Burunge WMAinayoundwa na vijiji kumi inazaa matunda wanatakiwa kushirikiana.
“Uendelevu wa Hifadhi hii ni kushikamana kwa ajili ya ulinzi wa shoroba na kuwadhibiti wale wavamizi na wanaotaka kutukwamisha lakini pia kuwadhibiti baadhi ya ambao watataka kuwahujumu tena”alisema.
Alisema Rais wa Jamuhuri ya Muungano, Dk Samia Suhulu Hassan anafanyakazi kubwa ya kutangaza Utalii ambayo imekuwa na manufaa makubwa hivyo, Burunge WMA ni lazima kuunga mkono jitihada za Rais kuvutia watalii lakini pia kuongeza mapato,kutokana na Utalii.
Afisa Wanyamapori mkoa wa Manyara,Felix Mwasenga na Afisa Wanyamapori halmashauri ya wilaya ya Babati, Christopher Laizer walieleza eneo la Burunge WMA ni muhimu sana katika utalii na Uhifadhi nchini ni lazima lilindwe lakini pia kuwa na mikakati na kuongeza mapato.
Mwenyekiti wa Burunge WMA,Erick Lilayoni alisema viongozi wote wa hifadhi hiyo, wamekubaliana kuondoa tofauti zao na tofauti zilizokuwepo na serikali na sasa wanashirikiana na mwekezaji wao chemchem ili kuendeleza uhifadhi na Utalii.
“Mkurugenzi wa halmashauri tunaomba radhi kwa yote yaliyotokea nyuma , tulitumika vibaya na kutaka kuyumbisha WMA lakini sasa tupo kitu kimoja na tunataka maendeleo”alisema.
Mjumbe wa bodi wa Burunge WMA,Lebrice Makau na Elibariki Lawasara waliomba radhi kwa serikali na halmashauri ya Babati kwani kwa miaka miwili walikuwa katika mgogoro baada ya kupotoshwa na hivyo, kushindwa kupokea ushauri ya wataalam.
Lawasara alisema wanamuomba radhi Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Mkuu wa wilaya Lazaro Twange na wataalam wote wa halmashauri na serikali kwa kupuuza ushauri wao kwa miaka miwili kwani walikuwa wamepotoshwa kwa maslahi ya wachache na sasa wamevunja makundi na wamekubaliana kushirikiana na serikali katika uhifadhi na kufata sheria zote.
No comments:
Post a Comment