Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam
Rais
Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amekipongeza Chuo
Cha Taifa ca Usafirishaji (NIT) katika Mpango wao wa kuanza kufundisha
Marubani wa Ndege, akibainisha hatua hiyo itasaidia kuongeza watenda
kazi katika sekta ya anga kwani ina uhaba mkubwa wa rasilimali watu.
Akizungumza katika Mahafali ya 39 ya NIT, Jakaya amesema kuwa ni ghali kwa kusomesha marubani nje ya nchi.
"Serikali
ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imenunua ndege mbili kwa ajili
ya mafunzo ya urubani, Injini mbili kwaajili ya mafunzo ya uhandisi wa
ndege na Cabin Crew mock ups kwa ajili ya mafunzo ya wahudumu wa ndani
ya ndege," alisema Rais Mstaafu.
Ameongezea:
"Aidha, Serikali imetoa ardhi katika eneo la Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) lenye ukubwa wa hekta 60, ambalo
litatumika katika kutoa Mafunzo ya Taaluma za Usafiri wa Anga.
Nimefurahi sana kuona uwekezaji huu mkubwa na muhimu kwa Chuo chetu,
hivyo, nitoe wito kwa Chuo, vifaa hivi ambavyo Serikali imenunua kwa
gharama kubwa vitunzwe ili Watanzania wengi wanufaike katika kupata
mafunzo."
Vilevile, JK aliwapongeza waitimu:
"Napenda
kuwapongeza sana nyote kwa jitihada mlizofanya wakati wote wa masomo
yenu hadi kufikia hatua hii ya kutunukiwa vyeti leo hii. Hongereni sana.
Ninatambua kuwa tuzo mtakayopata leo ni ya msingi kwenu katika safari
ndefu ya kuwa wataalam wazuri na mahiri. Ushauri wangu kwenu msiridhike
na ngazi ya taaluma mliyofikia, endeleeni kutafuta maarifa zaidi ili
Taifa liwe na wataalam wa kutosha na wenye sifa zote zinazohitajika
katika sekta ya Uchukuzi na Usafirishaji. "
Kwa Wanafunzi Mnaoendelea na Masomo, alisema:
"Katika
zama hizi ambapo kuna mabadiliko makubwa ya teknolojia hasa dunia
inapoingia kwenye Mapinduzi ya Nne ya Viwanda (4th Industrial
Revolution), ubunifu ni jambo muhimu kwa Nchi yetu katika kujenga
uchumi imara na stamihilivu. Hivyo, Wanafunzi mnaoendelea na masomo
kuweni wabunifu na kusoma kwa bidii ili mtakapohitimu masomo yenu muweze
kuwa na maarifa na ujuzi wa kutosha. "
Alisema
kuwa amefarijika sana kusikia kwamba Chuo kimeendelea kutanua wigo wa
kutoa mafunzo katika sekta hii muhimu ya Uchukuzi, ikiwa ni pamoja na
kujiimarisha katika Njia zote za Usafirishaji yaani Usafiri wa Anga,
Majini, Reli, Barabara na usafiri kwa njia ya mabomba.
"Nimefarijika
kusikia kuwa Chuo kikombioni kuanza kutoa Mafunzo ya Urubani. Mafunzo
haya ni muhimu sana kwa Taifa letu kwani yatapunguza mzigo kwa Serikali
na Wazazi wa kugharamia mafunzo haya nje ya nchi ambayo hutolewa kwa
gharama kubwa, " alisema.
Vilevile,
Jakaya alipata wasaa wa kuzindua Kitabu ambacho kimeeleza historia ya
Chuo tangu kuanzishwa kwake mwaka 1975 hadi kilipofika hapa.
"Nimefurahi
kuona sasa historia ya Chuo chetu imetunzwa vema kwani inatusaidia
kujua tulikotoka, tulipo sasa na wapi tuanataka kufika. Aidha, kitabu
hiki kinatunza historia ya Chuo kwa faida yetu, vizavi vijavyo na kwa
kwa ajili ya maendeleo ya taifa letu, " alisema.
Nae,
Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile alisema kuwa Katika kutekeleza
wajibu wetu wa kusimamia Chuo, Wizara imefanikiwa kusimamia uboreshaji
wa miundombinu na mazingira ya kufundishia na kujifunzia; uboreshaji wa
mafunzo yanayotolewa na Chuo; pamoja na kuimarisha rasilimali watu ya
Chuo.
Usimamizi
huu unalenga kukiwezesha Chuo kufikia malengo ya uanzishwaji wake, ili
kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa kama yalivyoainishwa kwenye Dira ya
Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025.
"Chuo
chetu kinatambua mapinduzi anuai ambayo Serikali ya Awamu ya Sita (6)
imeendelea kuyafanya kwa kuanzisha miradi mbalimbali katika sekta ya
Uchukuzi ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mipango mbalimbali ya nchi
ikiwemo Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo, Dira ya Taifa ya Maendeleo
ya mwaka 2025, Sera ya Taifa ya Uchukuzi ya mwaka 2003, pamoja na Ilani
ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020," alisema.
Amsisitiza
kuwa baadhi ya miradi hiyo ni ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), Ununuzi
wa Mabehewa na Injini za treni za kisasa, ujenzi wa Meli, upanuzi wa
Bandari, ujenzi na upanuzi wa Viwanja vya Ndege, ununuzi wa Ndege,,
ujenzi na upanuzi wa barabara pamoja na ujenzi wa Bomba la Mafuta Gafi
kutoka Hoima, Uganda kwenda Tanga, Tanzania.
"Mapinduzi
haya yameongeza mahitaji ya Rasilimali Watu yenye weledi wa hali ya juu
katika Sekta ya Uchukuzi nchini na ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki
na Kusini mwa Afrika," alisema.
Naibu
Waziri ametanabaisha "Hii inakifanya Chuo kubuni na kutoa mafunzo
yanayoendana na mahitaji ya soko ili kutoa wahitimu bora katika nyanja
zote za Usafirishaji (Barabara, Reli, Anga, Maji na Bomba). Hivyo basi,
katika Mpango Mkakati wa Nne wa Chuo wa Miaka Mitano (2021/2022 –
2025/2026), Chuo kitaendelea kuimarisha utoaji wa mafunzo yanayolenga
kuzalisha wataalam wenye ujuzi katika sekta ndogo zote tano za
usafirishaji kwa ajili ya ukuaji endelevu wa miradi hii ambayo
itachochea kwa kasi ukuaji wa Uchumi wa nchi yetu."
Kwa
upande wake, Kaimu Mkuu wa Chuo Dr Zainabu Mshana amesema kuwa Chuo
kimeendelea kuwajengea uwezo wahadhiri na watumishi wake kwa kuwapeleka
masomoni ili kuimarisha kiwango cha maarifa na ujuzi wao ambapo katika
mwaka wa masomo 2023/2024 jumla ya watumishi 71 wapo masomoni.
Amesema
kuwa kati ya hao, watumishi 39 wanasoma ngazi ya shahada ya uzamivu
(PhD), 24 wanasoma shahada ya uzamili, mtumishi mmoja (1) anasoma
shahada ya kwanza, Watumishi watatu (3) wanasoma Mafunzo ya Urubani na
Watumishi wanne (4) wanasoma Mafunzo ya Leseni ya Matengenezo ya Ndege.
Vilevile,
aliongezea kuwa katika kuimarisha na kurahisisha utendaji kazi, Chuo
kimefanikiwa kuhuisha muundo wake wa utumishi, ambao uliidhinishwa na
Mheshimiwa Rais tarehe 17 Novemba 2022 na umeanza kutekelezwa Mwezi
Oktoba 2023.
"Kwa
upande wa taaluma, Muundo huu una Vitivo vitano (5), Kurugenzi mbili
(2), Idara 14, Vitengo sita (6) na Vituo vinne (4). Kwa upande wa
Utawala, Muundo una Kurugenzi (5) na Vitengo vinne (4), "alisema.
Ameongeza
kuwa chuo hicho kimefanikiwa kufanya maboresho ya Muundo wake wa
Utumishi kwa kuongeza kada za wakufunzi wa usafiri wa anga na wahandisi
wa matengenezo ya ndege ili kuendena na matakwa ya sekta ya usafiri wa
anga. Muundo huu umeanza kutekelezwa mwezi Oktoba 2023.
Pamoja
na hayo, Chuo kimefanikiwa kuidhinishiwa Muundo wa motisha ili
kuboresha maslahi ya watumishi na kuongeza ufanisi wa kazi katika
shughuli mbalimbali za Chuo. Muundo huu umeanza kutekelezwa mwezi Julai
2023.
"Chuo
kina mikakati endelevu ya kutayarisha Rasilimali Watu watakaokidhi
mahitaji ya soko la ajira kwenye sekta ya Uchukuzi na Usafirishaji hasa
kwa kuzingatia utekelezaji wa mageuzi makubwa ya kiuchumi ambayo
Serikali ya Awamu ya sita (6) inayafanya, " alisema.
Alitaja
Mikakati hiyo ni Kuanzisha na kuhuisha mitaala ya kozi za mafunzo
mbalimbali kuanzia ngazi ya stashahada hadi shahada ya uzamili kuendana
na mahitaji ya soko la ndani na la nje ya nchi.
Na
vilevile kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia ikiwa ni
pamoja na ukarabati na ujenzi wa miundombinu ya madarasa, karakana,
maabara, ofisi na ununuzi wa vifaa vya mafunzo vinavyoendana na
mabadiliko ya teknolojia duniani.
No comments:
Post a Comment