Na Mwandishi Wetu, Tanga
WAZIRI wa Kilimo, Hussein Bashe, amesema mfumo wa kupima utendaji kazi wa maofisa kilimo sekta ya mkonge uko kwenye hatua za mwisho ambapo kila ofisa kilimo atapimwa kulingana na kazi alizofanya ikiwamo kuwatembelea wakulima shambani.
Akizungumza katika Mkutano wa Nne wa Wadau wa Sekta ya Mkonge uliofanyika mkoani Tanga hivi karibuni, Waziri Bashe amewataka maofisa kilimo kuacha kufanyakazi kwa mazoea na kuwafuata wakulima walipo.
“Tumewaletea mashine za kupima afya ya udongo na hivi karibuni tumepata fedha tunanunua magari kwa ajili ya maofisa kilimo tunataka wawe na magari bado vinakuja vishkwambi, halafu sasa nisikie mtu anabaki ofisini.
"...Lazima atapimwa mtu kutokana na kazi. Tunaweka mfumo, sasa ule mfumo unakamilika na lazima watu wajaze ripoti kila siku amemtembelea mkulima gani hata kama umemtembelea hujui tatizo utaweka kwenye mfumo aliyeko wizarani atajua hilo tatizo ni nini,” amesema.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba amebainisha ongezeko la wakulima wadogo wa mkonge mkoani humo inatokana hamasa inayoendelea kutolewa lakini pia ushirikiano mzuri wanaopata kutoka Wizara ya Kilimo.
“Hadi sasa Mkoa wetu una wakulima wadogo wapya wa mkonge 11,939 wameongezeka kufikia 2,245,000 mwaka 2021, hii inatokana na hamasa na ushirikiano ambao mmeendelea kutupa kama Wizara ya Kilimo tunawashukuru sana,” amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge (TSB), Saddy Kambona akizungumzia shamba la Kibaranga ambalo linamilikiwa na bodi hiyo, ameiomba Idara ya Ardhi Halmashauri ya Wilaya ya Muheza kuwapatia kanzidata na hati ya shamba hilo.
“Bado kumekuwa na mkanganyiko mkubwa kutoka kwa maafisa ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza kwa sababu wao ndiyo walikuwa na ile kanzi data ya wakulima ambao waligawiwa ardhi miaka ya nyuma ambayo tuliiomba waiwasilishe kwetu ili kuepusha migongano lakini hatukuweza kuipata hadi leo.
“Hati ilirudishwa wizarani na ikafutwa kwa hiyo lile shamba halina hati ila lilikuwa limekabidhiwa tu halmashauri kwa agizo la aliyekuwa Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi na sisi tulivyoliomba kwenye huo mchakato bado halijarudishwa kwetu kwa hati lakini kiutawala linaonekana lipo kwetu,” amesema Mkurugenzi Kambona.
Pamoja na mambo mengine, amesema wameanza ukarabati wa korona (mashine ya kuchakata Mkonge) ya Kibaranga kwa sababu baada ya kulichukua lile shamba bodi iliwasilisha maombi ya fedha wizarani kwa ajili ya ukarabati wa korona hiyo ambazo walipatiwa na kuanza kufanya mengine yanayolihusu lile shamba.
No comments:
Post a Comment