Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam
Asasi
ya Kiraia ya JamiiForums imezindua Awamu ya Nne ya Shindano la Stories
of Change ambalo litaanza rasmi Mei Mosi mwaka huu, na kuisha baada ya
miezi miwili.
Akizungumza
na wanahabari jijini humo Mkurugenzi Mtendaji wa JamiiForums Maxence
Melo amesema kauli mbiu ya shindano la mwaka huu itakuwa "Tanzania
Tuitakayo" ikilenga kuhamasisha wananchi kuibua mawazo mbadala ya nini
kifanyike kuipata Tanzania iliyo bora zaidi kwa kupendekeza mawazo
bunifu yanayoweza kutekelezeka ndani ya miaka mitano (5), 10, 15 hadi 25
ijayo.
"Katika
Mpango Mkakati wake wa miaka mitano (2020-2024), JamiiForums ilibuni
shindano la 'Stories of Change' lililoanza mwaka 2021. Na katika awamu
tatu zilizopita, takribani machapisho 6,000 yaliwasilishwa na wananchi.
Miongoni mwa maudhui yaliyowasilishwa, yamechangia kuboresha mifumo ya
utoaji huduma katika Sekta ya Umma na Binafsi," amesema Melo.
Amebainisha
kuwa shindano la mwaka huu asasi hiyo itashirikiana na mshirika wake wa
muda mrefu, Twaweza pamoja na wadau wengine kutoka Serikalini, asasi za
kiraia, mashirika yasiyo ya kiserikali na makampuni binafasi katika
nyanja mbalimbali kama habari, elimu, vijana, wanawake, watoto, makundi
maalumu, teknolojia, afya na kadhalika.
Amesisitiza
kuwa lengo ni kuimarisha ushiriki wa wananchi na utekelezaji wa maoni
ambapo amebainisha kuwa wadau hao ndio watakaoshiriki mchakato wa kupata
na kuwatuza washindi wa kisekta.
Amevitaja
vigezo na masharti ya kushiriki shindano hilo, ni kwamba mshiriki
anatakiwa kutayarisha andiko linakoelezea Tanzania Tuitakayo lenye maono
ya kibunifu ambayo yanaweza kutekelezeka ndani ya miaka mitano, 10, 15
hadi 25 ijayo katika nyanja mbalimbali mfamo elimu, afya, teknolojia,
uchumi, mazingira, miundombinu na kadhalika.
Kwamba
andiko liwe kwa lugha ya Kiswahili au Kiingereza lenye maneno kuanzia
700 hadi 100, kadhalika matumizi ya picha, vieo na vielelezo vingine
yanaruhusiwa ili kuongeza uzito wa wasilisho ambapo ikiwa picha au video
zilizotumika si za mshiriki atatakiwa kutaja chanzo.
Ameongeza
kuwa, machapisho yanatakiwa kuwa halisi na hayajawahi kuchapishwa
sehemu nyingine yoyote, kwamba ubwakuzi hautaruhusiwa na kueleza kuwa
maandiko yawasilishwe ndani ya miezi miwili kuanzia Mei 1, 2024 kwenye
jukwaa la "Stories of Change 2024".
"Ili
kushiriki, lazima mtu awe mwanachama aliyejisajili JamiiForums.com ili
kuchapisha andiko lake kwenye jukwaa la shindano la "Stories of Change".
Ikiwa sio mwanachama, anapaswa kujiandikisha kwa kufuata kiuongo hiki https://jamii.app/Signup," ameeleza Melo.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi wa Uchechemuzi wa Twaweza Annastazia Rugaba.
ametoa rai kwa wananchi wote wenye miaka 18 na kuendelea kushiriki
katika shindano hilo ili kutimiza haki yao ya msingi ya kuchangia mawazo
katika kujenga Tanzania Tuitakayo.
Amesema
washindi watatangazwa kwenye Jukwaa la JamiiForums "Stories of Change"
na kurasa rasmi za JamiiForums katika mitandao ya kijamii na X,
Facebook, Instagram, WhatsAPP na Telegram.
No comments:
Post a Comment