Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akizungumza katika uzinduzi wa mradi wa “Think Equal Lead Smart” uliofanyika jijini Dar Es Salaam Aprili 18, 2023.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya CEO Roundtable of Tanzania Santina Benson akitoa maelezo kuhusu mradi wa “Think Equal Lead Smart” wakati wa uzinduzi wa mradi huo uliofanyika jijini Dar Es Salaam Aprili 18, 2023.
Baadhi ya washiriki kutoka Taasisi mbalimbali nchini na nje ya nchi wakifuatilia mada mbalimbali wakati wa uzinduzi wa mradi wa “Think Equal Lead Smart” uliofanyika jijini Dar Es Salaam Aprili 18, 2023.
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa Taasisi ya CEO Roundtable of Tanzania na wadau wengine mara baada ya kuzindua mradi wa “Think Equal Lead Smart” uliofanyika jijini Dar Es Salaam Aprili 18, 2023. Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WMJJWM.
Na WMJJWM- Dar Es Salaam
Wanawake
nchini wameendelea kupata fursa za uongozi katika ngazi mbalimbali huku
takwimu zikionesha ongezeko la Wanawake katika uongozi ikiwemo Mawaziri
Wanawake kutoka asilimia 15 kwa mwaka 2005 hadi asilimia 37 kwa mwaka
2023. Aidha, Wabunge wanawake wameongezeka kutoka asilimia 22 hadi
kufikia asilimia 37 kwa mwaka 2023.
Hayo
yamebainika wakati wa uzinduzi wa mradi wa “Think Equal Lead Smart”
wenye lengo la kuhamasisha wanawake na vijana kushiriki katika nafasi za
uongozi na maamuzi uliofanyika jijini Dar Es Salaam Aprili 18, 2023.
Akizungumza
katika uzinduzi huo Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis amesema takwimu
zinaonesha pia Wanawake Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi
Zanzibar wameongezeka kwa asilimia 38, Madiwani asilimia 29.9. Mabalozi
asilimia 25, Makatibu Wakuu asilimia 22, Manaibu Makatibu Wakuu asilimia
28, Wakuu wa Mikoa asilimia 31, Makatibu Tawala asilimia 26, Wakuu wa
Wilaya asilimia 33 na Wakurugenzi asilimia 28.
Naibu
Waziri Mwanaidi amesema Tanzania imeendelea kutambua umuhimu wa
Wanawake kwa kuwapatia fursa katika nafasi za Uongozi na Maamuzi na
kuongeza ushiriki wao katika ngazi mbalimbali za Uwakilishi, Uongozi na
ngazi za maamuzi. Mabadiliko haya yanatokana na dhamira ya dhati ya
Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya kuhakikisha kuna usawa kati ya Wanaume na Wanawake na katika
nyanja zote.
Ameongeza
kuwa Wanawake wana mchango mkubwa katika maendeleo ya familia na Taifa
kwa ujumla, hasa ikizingatiwa kuwa kundi kubwa la watu nchini ni
Wanawake ingawa bado wanawake wanakabiliwa na changamoto zinazowaathiri
na kukwamisha maendeleo yao; miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na
uwepo wa mila na destruri zenye madhara, kutopatiwa fursa ya kupata
elimu pamoja na kutoshirikishwa katika shughuli za ujasiriamali na
uzalishaji mali.
"Serikali
inaendelea kusimamia utekelezaji wa mikataba ya Kikanda na Kimataifa
inayolenga kukuza Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji Wanawake hapa nchini.
Mikataba hiyo imekuwa chachu kwa maendeleo ya Wanawake ambapo kupitia
Jukwaa la Kizazi Chenye Usawa, nchi yetu inatekeleza afua mbalimbali
zinazochochea Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake Kiuchumi."
amesisitiza Naibu Waziri Mwanaidi
Aidha,
Naibu Waziri Mwanaidi amesema Serikali inatambua mchango wa Mradi huo
unaolenga kuwezesha ushiriki wa wanawake na fursa sawa za uongozi katika
ngazi zote za maamuzi nchini Tanzania na ameahidi kuendelea
kushirikiana Taasisi hiyo kuwafikia Wanawake hasa walio maneno ya
pembezoni mwa nchi.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya CEO Roundtable of Tanzania
Santina Benson amesema Taasisi hiyo imeanzisha mradi huo kwa lengo la
kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha Wanawake wanaoata
fursa sawa katika nyanja mbalimbali ikiwemo uongozi katika ngazi za
maamuzi na fursa za kiuchumi.
"Mradi
wa Think Equal Lead Smart (TELS) unaosimamiwa na Taasisi yetu unalenga
kuwezesha ushiriki wa wanawake na fursa sawa za uongozi katika ngazi
zote za maamuzi nchini Tanzania. Hivyo tunaomba Ushirikiano kutoka kwa
Serikali na Taasisi nyingine ili kufanikisha utekelezaji wa mradi huu
kwa pamoja" ameeleza Santina .
No comments:
Post a Comment