HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 15, 2024

BARABARA YA SENGEREMA -NYEHUNGE KM 54.5 KUJENGWA KWA KIWANGO CHA LAMI

Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey  Kasekenya amesema taratibu za kumpata mkandarasi mwingine ziko katika hatua za mwisho ili kuijenga kwa kiwango cha lami barabara ya Sengerema-Nyehunge KM 54.5 mkoani Mwanza.

Akizungumza katika ziara ya Katibu Mkuu wa CCM mkoani Mwanza wilayani Sengerema Naibu Waziri Kasekenya amesema zaidi ya shilingi bilioni 73 zinatarajiwa kutumika kwenye ujenzi huo ili kuyaunganisha kwa barabara ya lami majimbo ya Sengerema na Buchosa  na hivyo kuchochea shughuli za uvuvi, kilimo na biashara mkoani Mwanza.


Aidha Eng. Kasekenya amesema Serikali inaendelea na ujenzi wa barabara ya Sengerema-Kamanga KM 32 kwa wilayani Sengerema ambayo ujenzi wake unakwenda kwa awamu.

Pamoja na ujenzi wa barabara Serikali pia inajenga kivuko cha Buyagu-Mbarika ambacho ujenzi wake umefikia asilimia 55 ili kuunganisha wilaya za Sengerema na Misungwi na ujenzi wa kivuko kipya cha Kome-Maisome kitakachokuwa na uwezo wa kubeba tani 170 na magari 22 na hivyo kupunguza adha ya usafiri wilayani Sengerema.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa CCM Dkt. Emmanuel Nchimbi ameipongeza Wizara ya ujenzi kwa kasi ya ujenzi wa daraja JP Magufuli Kigongo-Busisi lenye urefu wa Km 3 na barabara unganishi km 1.6 na kuzungumzia umuhimu wa kuweka alama zote za tahadhari katika daraja hilo kubwa nchini pindi litakapokamilika.

Amesisitiza umuhimu wa Wizara kuimarisha uwezo wa kuwapima vizuri wakandarasi kabla ya kuwapa mikataba ya miradi ili kuharakisha ujenzi wa miundombinu.

" Hakikisheni mnapata wakandarasi makini ili miradi ijengwe kwa wakati na ubora na hivyo kuleta tija kwa wananchi", amesisitiza Balozi, Dkt. Nchimbi.

No comments:

Post a Comment

Pages