HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 24, 2024

Waziri Mavunde: Mkutano wa Kimataifa wa Sekta ya Madini kufungua Fursa za Uwekezaji Nchini

Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam

Sekta ya Madini Tanzania imekuwa ikivutia kwa Wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali ambao wanatarajiwa kushiriki Mkutano wa 5 wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini, utakaofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Novemba 19 hadi 21 mwaka huu. 

Akizungumza na wanahabari Jijini humo wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Mkutano huo Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesema  mkutano huo utaleta pamoja wadau wa kimataifa katika sekta ya madini hivyo kuendelea kutangaza sekta ya Madini ya Tanzania.

Amebainisha kuwa mkutano huo utahudhuriwa na wadau mbalimbali toka nchi tofauti Duniani wakiwemo Wawekezaji wa Madini, Watafiti wa Madini, Wachimbaji, Wawakilishi wa Serikali, Viongozi kutoka Mataifa ya kigeni, Wawakilishi na Mabalozi wa nchi mbalimbali kwa pamoja wakilenga kujadili fursa za kipekee za Uwekezaji katika uongezaji thamani madini, uchimbaji na hususan wakati huu ambapo mahitaji ya madini muhimu yanaongezeka duniani.


“Ni maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwamba madini yote yanayochimbwa hapa nchini ili kuongeza mchango wa Sekta katika Pato la Taifa, kulinda na kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania, kuchochea ukuaji wa teknolojia katika Sekta, kuchochea maendeleo ya jamii na uchumi kwa ujumla” amesema Waziri Mavunde na kuongeza kuwa,

“Kaulimbiu ya mkutano huu ni, Uongezaji  Thamani  Madini kwa Maendeleo ya Kijamii na Kiuchumi hivyo mkutano huo utakuwa jukwaa muhimu la majadiliano ya kina yatakayotoa mwelekeo mpya kwa sekta ya madini nchini, huku ukiibua fursa mpya za uwekezaji na uhamishaji wa teknolojia.

Hata hivyo amesema, Mkutano huo pia unatarajiwa kuwa fursa ya kipekee kwa washiriki kufahamu Sera za Madini za Tanzania, vivutio vya uwekezaji, na mipango ya serikali ya kuboresha mazingira kwa ajili ya kuvuna madini kwa maendeleo endelevu. 

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo amefafanua kuwa mkutano huo utakuwa msingi wa kujenga uwezo na uhamishaji wa teknolojia kupitia majadiliano ya kina ya kitaalamu na mawasilisho ambayo yatatoa mwelekeo mpya kuhusu jinsi ya kuboresha sekta, pamoja na kutafuta fursa mpya za kuongeza thamani ya madini. 

“Mkutano huu pia utatoa fursa za uwekezaji kwa kuvutia zaidi kampuni za utafiti, uchimbaji, usindikaji na uongezaji thamani madini, na watoa huduma ili kuchimba na kuongeza thamani madini muhimu na vito vinavyopatikana Tanzania” ameongeza Mbibo

Nae, Mtendaji Mkuu wa Chemba ya Migodi Tanzania, Mhandisi Benjamin Mchwampaka amesema kuwa wao kama Chemba ya Migodi wanaishukuru Wizara ya Madini kwa kuwachagua kushirikiana kwa pamoja katika kuandaa mkutano huo.

“Sisi ndio sauti ya Wawekezaji katika Sekta ya Madini hapa nchini, tunaamini kuwa mkutano huu utatuongezea ufanisi katika namna ya uendeshaji wa shughuli zetu za kila siku na mnyororo mzima wa Sekta ya Madini, pia kupitia ushirikiano huu tunaamini tutakuwa na Mkutano mzuri mwezi Novemba 2024” amesisitiza Mhandisi Mchwampaka. 

Sambamba na hayo Mkutano huo utaambatana na Usiku wa Madini ambao utahusisha Maonesho ya Vito yenye lengo la kutangaza utajiri mkubwa wa Tanzania katika madini ya vito sambamba na tukio la kuwatambua kampuni na wachimbaji waliofanya vizuri kwa kipindi kilichopo.

No comments:

Post a Comment

Pages