HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 26, 2024

Eda Sanga na mumewe Lazarus Sanga washerehekea Jubilei ya dhahabu ya ndoa yao

Siku Bi Eda William Ngurukuru Sanga na  Lazarus Abel Sanga walipofunga ndoa miaka 50 iliyopita.

Siku Bi Eda William Ngurukuru Sanga na  Lazarus Abel Sanga waliposherehekea miaka 50 ya ndoa.

Baba Paroko alikuwepo kuwabariki Bi Eda William Ngurukuru Sanga na  Lazarus Abel Sanga kwa kusherehekea miaka 50 ya ndoa.

Bi Harusi akiwa na Mwenyekiti wa TAMWA na mtangazaji maarufu Joyce Shebe, na Mkuu wa Wilaya mstaafu na mtangazaji Bakari Msulwa.

Ankal na Maharusi.

Manju wa Muziki Masoud Masoud na maharusi

Maharusi wakiwa na Balozi Charles Sanga na mkewe pamoja na Mwenyekiti wa TAMWA na mtangazaji maarufu Joyce Shebe na ndugu.

Maharusi wakiwa na Balosi Charles Sanga na mkewe.

Maharusi na watoto wao mapacha, Kurwa (kulia) na Dotto.

Maharusi na ndugu, jamaa na marafiki.

PICHA NA HABARI NA ISSA MICHUZI

Ni Ijumaa Oktoba 25, 2024 jioni, hususan katika sherehe ya maadhimisho ya Jubilei ya Dhahabu katika kitongoji cha Segerea, Dar es Salaam. Bi Eda William Ngurukuru Sanga, gwiji wa utangazaji nchini Tanzania, alikuwa kitovu cha kila kitu, akiwa amesimama kando ya mumewe, Lazarus Abel Sanga.

Wawili hawa wapendanao walikuwa wakisherehekea miaka hamsini—ndiyo, miongo mitano mizima—ya ndoa. Kwa yeyote anayemfahamu, Eda Sanga si tu mtangazaji mkongwe; bali pia ni nguzo ya uanzilishi wa taasisi kadhaa na mwalimu aliyetukuka wa wanahabari wengi sana nchini humu katika fani ya utangazaji.

Kabla hajastaafu alikuwa Mkurugenzi wa Utangazaji wa iliyokuwa Taasisi ya Utangazaji Tanzania (TUT) na sasa TBC, na pia mmoja wa waanzilishi 12 na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) mstaafu.

Pia Eda Sanga ni Mtangazaji mkongwe nchini ambaye ni miongoni mwa wanawake wachache waliosikika wakitangaza mwanzoni kabisa  kupitia Tanganyika Broadcasting Services (TBS) kabla haijawa iliyokuwa Radio Tanzania Dar es salaam (RTD) na sasa (TBC Taifa). Pia alihudumu kama  Meneja wa vyombo vya habari vilivyo chini ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam, akiwanoa vijana wanaopiga kitabu katika Shule Kuu ya Uandishi wa Habari kabla hawajajichovya kwenye bahari ya ajira.

Hakika sherehe hii ilikuwa na utofauti wake na ya kihistoria. Kwa mara ya kwanza watu wameshuhudia dunia ya Eda nje ya kazi, na kwa siku moja, akiwakaribisha marafiki, familia, majirani na hata wenzake kushiriki kwenye tukio la maisha yake binafsi. Sio la kiofisi!

Kwa mtu ambaye sauti yake imekuwa sehemu ya mawimbi ya redio nchini, unaweza kudhani kwake yeye kazi tu ndio ni kila kitu. Lakini hapa alikuwa akithibitisha kwamba fanya ufanyalo katika maisha yako lakini daima weka nafasi ya upendo na furaha kwa kuwa karibu na familia yako.

Sherehe hii ilinogeshwa na mchanganyiko wa nyuso za marafiki wa zamani na wanahabari kadhaa waliofuatana naye katika safari ya utangazaji. Miongoni mwa wageni alikuwepo kaka yake Eda mwenyewe, Balozi Charles Sanga, ambaye yeye pia anajulikana kwa umahiri katika medani ya diplomasia. Alikuwepo pia Mwenyekiti wa TAMWA na mtangazaji maarufu Joyce Shebe, Mkuu wa Wilaya mstaafu na Mtangazaji Bakari Msulwa,  na Manju wa Muziki Masoud Masoud, pamoja na “Ankal” Issa, aliyekuwa akikoleza shamrashamra kwa upigaji picha na vichekesho juu.

“Maharusi” Eda na Lazarus, walikata keki mbele ya kila mtu, wakiwa na tabasamu, huku wakifurahia joto na shangwe za wageni. Kisha, kama ilivyo ada katika  sherehe yoyote ya Kitanzania, muziki ulichukua nafasi yake. Wapenzi hao walilishana keki, na kusakata muziki kwa furaha, huku wageni wao wakiwapongeza kwa vifijo na vigelegele. Hapa ungemuona jinsi Eda Sanga alivyokuwa akicheza twist ya “Kondakita nipe Tiketi” hadi chini, usingeamini macho yako. Na hapo jinsi alivyoupuna na kupendeza na taji la Bi harusi kichwani ungezimia kabisa. Ungejiuliza kuumbe hata watu walio serious na kazi ni binaadamu kama wengine.

Kusema kweli hii haikuwa tu sherehe; ilikuwa ni ishara ya uvumilivu, ushirikiano, na mapenzi ya kudumu yaliyopandwa na kukuzwa kwa miaka hamsini. Vile vile iliendeleza mila na desturi za Kitanzania za watu kuishi pamoja kama mume na mke, hata kama wametokea sehemu tofauti za nchi. Eda ni mzaliwa wa  Sengerema mkoani Mwanza ila kakulia mkoani Iringa. Lazarus ametoka Songea, mkoa wa Ruvuma….

Kwa wale waliokuwepo, ilikuwa dhahiri: mafanikio ya Eda hayapo katika kazi tu, bali pia katika uwezo wake wa kuwaleta watu pamoja. Ilikuwa Jubilei ya Dhahabu iliyostahili, na kwa jinsi walivyoonekana, ni dhahiri kwamba  bado ngoma nyingi za kucheza ziko mbeleni mwa wawili hawa.

No comments:

Post a Comment

Pages